NA TIGANYA VINCENT
VIONGOZI wa Dini Mkoani Tabora wameiomba Serikali kutowaonea aibu wale wote wanaoleta mzaha na wanaotafuta umaarufu kupitia janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoeneza na kirusi kipya aina ya Corona Covid-19.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa maombi na dua maalumu Viongozi wa Dini na Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuuweka Mkoa wa Tabora ,Taifa na Dunia nzima mikononi mwa Mungu ili awakinge na janga la ugonjwa wa Corona.
Mchungaji wa Kanisa la Agape Miracle Centre Elias Mbagata alisema bado kuna kuna mizaa inaendelea juu ya janga hili hivyo ameiomba serikali isiwaonee haya wanoendekeza hayo hata kama ni viongozi wakubwa wakiwemo wa Dini.
Alisema kinachotakiwa kufanywa kwa sasa ni kuwajengea matumaini wananchi badala ya kuwajaza hofu ambayo itawasababisha wachanganyikiwe.
Askofu wa wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Dk Elias Chakupewa alisema wameshachukua hatua mbalimbali za kuwaelimisha waumini wao kufuata taratibu zote zinazotakiwa ikiwemo maelekezo ya wataalamu na viongozi wa Serikali namna sahihi ya kujikinga na janga la Covid -19.
Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Tabora Mhashamu Paul Ruzoka aliwaomba waumini kuungana na serikali katika kupigana vita hii iliyo mbele yao kwa kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yanayotolewa na viongozi pamoja na wataalam wa afya.
Alisema Kanisa hilo limesitisha kwa muda baadhi ya taratibu za uendesha wa Ibada ikiwa ni seehemu ya mikakati ya kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya Covid -19.
Kwa upande wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi aliwashauri viongozi wa Dini kuendelea kushirikiana na serikali na kufuata maelekezo ya wataalamu katika kuhakikisha wananchi na waumini wao wanapata maelekezo sahihi kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo hatari.
Askofu wa Kanisa la Morovian Tanzania Magharibi Ezekiel Yona alisema wao kwa kutambua ukubwa wa tatizo wametoa jingo katika Hospitali yao ya Sikonge kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa Covid -19 kama kwa bahati mbaya wataonekana.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Magharibi Kati, Askofu Isaac Laizer alimpongeza Rais Dokta John Pombe Magufuli kwa kwa kuthubutu kuitangazia dunia kwamba janga la ugonjwa wa Corona litamalizika kwa wananchi watakapokubali kumuomba Mungu.
Alisema wao wanaungana na Serikali kwa kusimamisha baadhi ya huduma ikiwemo ya mafunzo kwa watoto wadogo (Sunday school) na kualika wataalamu kutoa elimu ya kujikinga na Corona.
Viongozi hao wamadhehebu ya dini wamesema kwamba pamoja na serikali kuchukua taadhali inabidi wananchi kumlilia Mungu ili awasamehe dhambi na kuwaepusha na janga hilo.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwashukuru viongozi hao wa kiroho kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali na kuwaomba wasaidie kufikisha elimu kwa waumini wao ili isaidie kuuepusha Mkoa huo na janga la Covid 19.
Social Plugin