Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU MANYARA YAMFIKISHA MAHAKAMANI MTENDAJI WA KIJIJI KWA KUOMBA RUSHWA SH. 50,000

Na John Walter- BABATI

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoa wa Manyara imemfikisha mahakamani afisa mtendaji wa Kijiji cha Gichameda  John Bura kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu hamsini (50,000).

Mwendesha mashtaka wa Takukuru Eveline Onditi alisema shauri hilo namba 94 limetajwa kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa Manyara Jumaa Mwambago.

Onditi alisema kuwa Machi 31,2020 katika stendi ya Matufa afisa mtendaji wa Gichameda akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya wilaya ya Babati alimuomba rushwa ya shilingi 50,000 Husein Darabu  ili aweze kumpatia utambulisho wa kwenda kupata dhamana ya mdogo wake ambaye alikuwa kituo kidogo cha polisi Magugu.

Onditi ameeleza kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kugoma kumuandikia barua ya utambulisho Husein Darabu ambaye alikuwa anaenda kumdhamini mdogo wake aliyekuwa anashikiliwa na polisi kituoni hapo.

Amesema Darabu baada ya kuombwa rushwa alifika ofisi za Takukuru na kutoa taarifa ndipo mtuhumiwa aliwekewa mtego na kukamatwa.

Ameyataja makosa ya mtuhumiwa kuwa ni kuomba na kupokea rushwa kinyume na matakwa ya mwajiri wake na kosa jingine ni kuomba na kupokea rushwa.

Onditi amesema mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 kifungu cha 15.

Aidha mshtakiwa alisomewa mashtaka Aprili 2, 2020 na amekana makosa yote na amepewa sharti la dhamana kuwa ni lazima awe na mdhamini na kutoa shilingi laki tano (500,000) ambayo ameitoa yote na kuachiwa huru.

Hata Hivyo shauri hilo limeahirishwa mpaka litakapotajwa tena Aprili 30,2020 kwa ajili ya kusikilizwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com