THTU YATOA MAPENDEKEZO KADHAA YA KUKABILIANA NA ATHARI ZITOKANAZO NA JANGA LA CORONA


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania(THTU) Dkt.Paul Loisulie (kushoto) akizungumza wakati akitoa taarifa yake kwa wanachama wake, wadau na umma wa watanzania wote nchini ikiwa ni sehemu ya kuungana na serikali katika kupigana vita dhidi ya Corona.
............................................................................................
“Ni Wajibu wa Kila Mmoja Wetu: Jilinde na Mlinde mwenzako, Timiza wajibu wako kwa,
pamoja tutazuia corona”
  1. Utangulizi
Ugonjwa wa corona (Covid 19) umeleta athari kubwa duniani katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Pia umeharibu utaratibu na mfumo mzima wa maisha ya kawaida katika nchi zote na kusababisha maelfu ya vifo duniani. 

Serikali na Wataalamu wa afya wameelekeza njia mbalimbali za kujikinga na kuepuka ugonjwa huu ambao mpaka sasa hauna tiba. 

Njia hizo ni pamoja kuepuka mikusanyiko, kutumia vitakasa
mikono, kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka, kutosafiri au kwenda sehemu yoyote yenye watu wengi isipokuwa kwa mahitaji ya muhimu, na kuwekwa
karantini kwa wale wote wanaohisiwa kuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo. 

Serikali ya Tanzania, kama zilivyo serikali nyingi duniani, imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti njia za maambukizi ya ugonjwa huu zikiwemo zuio/katazo la shughuli nyingi zenye mikusanyiko mikubwa kama vile michezo, matamasha, makongamano na aina
nyinginezo zinazofanana na hizo.

 Pia shule zote za awali, msingi na sekondari pamoja
na vyuo ngazi zote zimefungwa kwa muda usiojulikana.

THTU inapongeza hatua zote za kiafya ambazo zimechukuliwa na serikali na wataalamu mbalimbali wa afya mpaka sasa na pia tunaunga mkono michango
mbalimbali ya mawazo ya kitaalamu inayotolewa na taasisi mbalimbali au mtu mmoja mmoja katika kukabiliana na janga hili.


 Hivyo basi, kwa kuzingatia hali hii inayoendelea
duniani kote na ndani ya nchi yetu, sisi THTU kwa kutumia kauli mbiu yetu ya “Nia na
1
Mwelekeo ni Kujenga Daima, Taifa Kwanza” tumeamua kutoa mchango wa maoni yetu
ya namna ya kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa corona pamoja na
ushauri wa namna ya kukabiliana na athari zilizojitokeza na zitakazojitokeza.
  1. Namna ya kuendeleza Mapambano dhidi ya corona;
  1. Kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu na uelewa wa kila mwananchi mmoja
mmoja kuhusiana na ugonjwa huu, tunashauri kuongezwa kwa kampeni na
hamasa kubwa kwa mtu mmoja mmoja maeneo yote nchi nzima ili kuongeza
uelewa na umakini katika kudhibiti corona.
  1. Kuimarisha dhana ya serikali shirikishi kwa ngazi zote za Tawala za mikoa
(Mikoa na Wilaya) na serikali za mitaa (Halmashauri za Majiji, Manispaa, Wilaya,
mamlaka ya miji, kata na Vjiji/Mtaa) ili kuwezesha wananchi kuchukua hatua
stahiki za kujikinga na ugonjwa huu na pia kutoa taarifa pale wanapoona kuna
wananchi wenye dalili za ugonjwa huu.
  1. Viongozi wa dini zote wachukue hatua madhubuti ya kuwalinda waamini wao
kwa kutafuta njia mbadala ya kufanya shughuli za kiimani isiyohusisha
mikusanyiko. Ikiwezekana hatua zilizochukuliwa na Maaskofu wawili wa Mkoa
wa Kagera (Mhashamu Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la
Rulenge – Ngara na Mhashamu Askofu Benson Bagonza wa KKKT Dayosisi ya
Karagwe) zifanyiwe kazi na viongozi wengine wa dini zote ili kuendeleza
mapambano dhidi ya corona. Sisi THTU tunaamini kuwa pamoja na maombi kwa
Mwenyezi Mungu kupitia Imani zetu za kidini, bado jitihada za kisayansi lazima
zichukuliwe na kila mmoja wetu.
  1. Katika kipindi hiki, tunapendekeza taasisi mbalimbali za serikali na zile za binafsi
kuruhusu baadhi ya wafanyakazi wao kufanya kazi kwa kutokea nyumbani ili
kupunguza mikusanyiko ya wafanyakazi maeneo ya kazi na kubaki na
wafanyakazi wachache sana ambao ni muhimu kuwepo ofisini ili kuendelea
kulinda utendaji wa taasisi hizo. Mfano, maeneo ya Vyuo Vikuu, vyuo vya kati na
shule, katika kipindi hiki ambacho wanafunzi hawapo, baadhi ya wafanyakazi
2
wangebaki nyumbani na kutumia mtandao wa intaneti kuwasiliana kwa shughuli
mbalimbali za kiofisi.
  1. Kwa siku za hivi karibuni, taarifa za serikali zimeonyesha kuwa maambukizi
yanaongezeka yakiambatana na vifo. Hivyo basi ni ushauri wetu kuwa hatua za
kupiga marufuku shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko ya watu ziendelee
kuimarishwa kwani ushauri wa kitaalamu unaonyesha mikusanyiko ni njia moja
kuu inayosababisha kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa huu.
  1. Katika nyakati hizi ambazo kila mwananchi yuko katika jitihada za kulinda afya
yake na wale walioko karibu yake na kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za
kiafya kwa kila mmoja wetu, tunashauri kuwa Taasisi mbalimbali ziepuke kutoa
taarifa au kufanya maamuzi yanayoleta au kuongeza msongo wa mawazo kwa
watu hasa katika nyakati hizi za janga la corona. THTU kwa masikitiko makubwa,
imeshtushwa na hatua zilizochukuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) kupitia taarifa yao ya tarehe 14/04/2020 kuhusu wanufaika wa huduma za
bima ya afya ambao ni watoto wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Kwa
maoni yetu, taarifa hii imeleta usumbufu mkubwa kwa wanufaika wa bima ya
afya wakiwemo wanachama wa THTU ambao ni wachangiaji katika mfuko huo.
  1. Tunashauri kuwa ni vema Mfuko wa Bima ya Afya ukaonesha uungwana kwa
kusitisha uamuzi wao huo kama njia ya kuunga juhudi za kupambana na janga la
corona kwa kuwapa uhakika wanachama wake kuweza kupata huduma za afya
kwa wategemezi wao hao na hali ya nchi ikitengamaa wakae na wadau ili kujadili
namna njema ya kufanya mabadiliko hayo. Kila mmoja anaelewa mfumo wetu
wa afya ulivyo na namna ambavyo wananchi wengi wanaoishi na wategemezi
wao wanavyotegemea huduma za afya zilizopo. Kufanya maamuzi hayo katika
kipindi hiki ni kuwaongezea wanachama wa Mfuko huo msongo wa mawazo na
mzigo mkubwa wa kiuchumi katika nyakati ambazo hali ya kiuchumi ni mbaya
kutokana na athari za ugonjwa huu wa corona.
3
  1. Utengenezaji wa vitakasa mikono (hand sanitizers), barakoa na vifaa vingine
usimamiwe na mamlaka zinazohusika ili zikidhi vigezo vinavyotakiwa lakini pia
ziuzwe kwa bei ambayo watu wote wanamudu. Wafanyabiashara wasio
waaminifu wanaweza wakatumia mwanya huu kujinufaisha bila kujali uhai wa
watu.
  1. Mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa nchi kavu (LATRA) ikishirikiana na Jeshi la
Polisi kitengo cha usalama barabarani iongeze usimamizi wa maelekezo ya
wataalamu wa afya katika usafiri wa umma kipindi hiki cha hili janga.
Ikiwezekana kwa sasa jitihada kubwa zielekezwe kwenye usimamizi wa
maelekezo hayo ili kusaidia kupunguza maambukizi.
  1. Vyombo vya habari kwa ujumla wake (redio, televisheni na magazeti) pamoja na
mitandao ya kijamii vimefanya kazi nzuri mpaka sasa. Lakini tunashauri kuwa
ubunifu zaidi wa vipindi na makala ya kusaidia mapambano dhidi ya corona
uongezwe kwa kuongeza matanagzo yenye elimu ya kujikinga na ugonjwa wa
corona katikati ya vipindi vinavyopendwa na watu wengi. Utoaji wa taarifa sahihi
ni muhimu sana katika kipindi hiki. Vyombo vya habari vina nafasi ya pekee
kabisa katika hili.
  1. Ushauri wa namna ya kukabiliana na athari zinazotokana na janga la corona:
Pamoja na jitihada za kudhibiti na kutokomeza gonjwa hili la corona, ni ukweli
usiopingika kwamba tayari athari zimeshaonekana na nyingine zitaonekana siku zijazo.
Hatupaswi kuendelea kusimama katika taratibu za kawaida tulizozoea wakati corona
imeshavuruga taratibu hizo. Ni lazima tujipange na kutafuta utaratibu mbadala wa
kukabiliana na athari za sasa na zijazo. Tukitambua ukweli kwamba ni lazima maisha
yaendelee sambamba na mapambano ya huu ugonjwa, sisi THTU tunatoa
mapendekezo ya namna ya kukabiliana na athari kama ifuatavyo;
  1. Vyuo vikuu, taasisi za elimu ya Juu na vyuo vya kati vioneshe umahiri wao wa
kutumia fursa za TEHAMA kuhakikisha kwamba vipindi vinaendelea kwa yale
masomo yanayowezekana kwa njia ya mtandao. Hii ni njia mbadala ambayo
4
itasaidia taasisi hizi kupangilia vizuri mihula ya masomo pale ugonjwa huu
utakapodhibitiwa. Kukaa kusubiri tatizo liishe ndipo kuchukua hatua ni
kutojitendea haki wenyewe, kutoitendea haki jamii na nchi kwa ujumla. Wito wetu
kwa serikali ni kuwezesha taasisi hizi kuweza kufanikisha malengo haya na
kutoa msaada kwa taasisi za binafsi ambazo kwa wakati huu zinapitia wakati
mgumu sana kufuatia vyanzo vyao vikubwa vya mapato kusimama kutokana na
wanafunzi wengi kutolipa ada kwa wakati huu.
  1. Utaratibu ulioanzishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania ya utoaji wa elimu
mtandaoni na kwenye televisheni uboreshwe zaidi kwa kuhusisha redio ili
kuwafikia wanafunzi wote nchi nzima. Ili kutoharibu mtiririko wa mihula,
wanaweza wakatafutwa walimu wa kila somo na kurekodi vipindi (mada zote)
ambazo zitarushwa kwenye redio zote nchi nzima na wanafunzi kutakiwa
kusikiliza na kufanya majaribio. Hili litasaidia kuwafikia wanafunzi wote nchi
nzima. Hoja ya msingi hapa ni kurasimisha utaratibu wa utoaji wa elimu kupitia
mitandao, vyombo vya habari (redio, televisheni na mitandao ya kijamii) hasa
wakati huu wa janga la corona.
  1. Makampuni ya simu yaliyopo Tanzania yanashauriwa kutafuta namna ya
kupunguza gharama za vifurushi vyao vya intaneti na pia miamala yao wakati
huu wa corona ili kuruhusu watu wengi kufanya malipo kwa kutumia mitandao ya
simu bila kuhofia gharama. Pesa ambayo huwa inatumika kutimiza azma ya
wajibu kwa jamii (corporate social responsibilities) inaweza kusaidia kutumika
kwa njia hii ya kupunguza gharama za miamala na vifurushi.
  1. Wizara zote zijielekeze katika kutengengeza taratibu na mazingira wezeshi
yatakayoendelea kulinda mazingira ya kiuchumi na kijamii kwa mwananchi wa
kawaida na pia kulinda shughuli za kiuchumi za biashara mbalimbali ili kulinda
ajira za wafanyakazi wengi.
  1. Taasisi za elimu ya Juu na vyuo vikuu vichukue hatua ya kufanya tafiti na
machapisho juu ya ugonjwa huu wa corona badala ya kusubiri machapisho na
5
tafiti kutoka vyuo vya Ulaya na Marekani. Hatua hii itasaidia sana kuwepo kwa
taarifa sahihi za dunia na za mazingira yetu pia.
  1. Ni wakati muafaka wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kutekeleza dhana
ya Tanzania ya viwanda kwa kupambana kutengeneza bidhaa zitakazouzwa
ndani na nje ya nchi ili kuondoa upungufu wa bidhaa na huduma zilizokuwa
zinaletwa kutoka nje ya Tanzania kabla ya janga la corona. Tunashauri serikali
kufanya jitihada za makusudi kulinda viwanda vyetu vya ndani ili visifungwe na
hivyo kuhatarisha mapato ya ndani na ajira za wafanyakazi wengi.
4.Hitimisho
Mapambano dhidi ya janga la corona si ya serikali, mtu mmoja au kundi moja.
Tunahitajika kufanya kazi kwa ushirikiano kuanzia mtu binafsi mpaka jamii yote kwa
ujumla. Serikali na Wataalamu wa afya peke yao hawataweza kufanikisha vita dhidi ya
janga la corona kama jamii itaendelea kuishi maisha kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Pamoja na Imani zetu za kidini, maombi peke yake bila tahadhari haiwezi kudhibiti
corona. Ni vyema tufuate ushauri wa wataalamu, tuunganishe nguvu zetu pamoja. Huu
ni wakati wa kuchukua hatua zitakazoendelea kuimarisha umoja wetu watanzania,
kuelimishana, kupunguziana ugumu wa maisha na kupeana moyo huku tukipena taarifa
sahihi juu ya corona. Kwa pamoja tutashinda.
NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA, TAIFA KWANZA
Dkt. Paul Loisulie
MWENYEKITI THTU TAIFA
6

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post