UGANDA KUMREJESHA NCHINI MTANZANIA ALIYEKUTWA NA CORONA


Wizara ya Afya ya Uganda imesema kuwa itamrejesha nchini Mtanzania aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo katika mpaka wa Mutukula.


Aprili 17 wizara hiyo ilithibitisha kisa kimoja ambapo taarifa ya awali ilieleza kuwa maambukizi hayo yametokea miongoni mwa jamii nchini humo, taarifa ambayo baadae ilikanushwa kuwa haikuwa sahihi.

Katika taarifa mpya wizara hiyo imesema aliyebainika kuwa na maambukizi hayo ni dereva wa lori mwenye miaka 34 ambaye ni raia wa Tanzania, na aliwasili Mutukula Aprili 16 akitokea jijini Dar es Salaam.

Dereva huyo hakuwa na dalili yoyote yenye kuonesha kuwa alikuwa na maambukizi ya homa ya mapafu (COVID-19), na sasa jitihada za kumtafuta na kurejesha nchini Tanzania zinaendelea, wizara imesema.

Kutokana na msahihisho hayo, visa vya watu wenye maambukizi ya COVID-19 nchini Uganda vinabaki kuwa 55.


Hatua ya Uganda kuwarudisha nyumbani raia wa kigeni waliopatikana na ugonjwa wa corona imezua gumzo kali katika mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi hiyo.

Siku ya Alhamisi waziri wa Afya wa Uganda  Ruth Jane Aceng alisema kuwa Uganda kila siku huwapokea hadi madereva 3,000 wa malori kutoka mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki na kwamba nchi hiyo haitaweza kuwapa huduma za matibabu. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post