Wabunge Wameendelea kutoa michango ya Maoni yao kuhusu hotuba ya mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi za Ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021 iliyowasilishwa hapo April 1,2020 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku wakiitaka serikaka kuweka kipaumbele zaidi katika kutoa elimu ya kujikinga na Corona kwa makundi ya watu wenye ulemavu wakiwemo wasioona.
Wakichangia maoni mbalimbali bungeni jijini Dodoma akiwemo Mbunge wa viti Maalum ,Amina Mollel amesema katika mapambano dhidi ya Virusi vinavyosababisha na homa kali ya mapafu ,Corona[COVID-19]elimu inahitajika kwa kina zaidi kwa watu wenye ulemavu hususan vipofu.
“Watu wasiokuwa na ulemavu elimu ni rahisi kutolewa ,mfano kumwonesha namna ya kunawa mikono,kwa kutumia sanitizer ,Kwa hawa wenzetu wenye ulemavu wanapata changamoto kubwa sana hivyo ninaomba serikali iweke kipaumbele zaidi katika kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ,mfano mlemavu wa macho [kipofu]haoni chochote kinachoendelea bila elimu kwa kina ni changamoto kwake”amesema.
Kwa upande wake mbunge wa Korogwe Mjini Mhe.Mary Chatanda ambaye pia ni Kamishna wa Huduma za Bunge amesema maelekezo yanahitajika zaidi kwa wananchi juu ya tahadhari ya Corona huku mbunge wa viti maalum Mhe.Hadija Nasiri Ali anayewakilisha kundi la vijana Bungeni akitoa ushauri kwa serikali kupunguza masharti kwa taasisi za kifedha ili vijana wengi zaidi waweze kujiajiri.
Mbunge wa Njombe Mjini Mhe.Edward Franz Mwalongo amesema serikali inatakiwa kuwaandaa zaidi wananchi kuhusiana hali ya corona ilivyo duniani na hali ikiendelea kuwa mbaya watu wajifungie ndani.
Kuhusu idara inayohusika na ujuzi Mhe.Mwalongo ameomba idara hiyo ipanue zaidi katika maeneo ya vijijini kwenye sekta za kilimo na ufugaji kwani imekuwa ikijikita katika sehemu za mjini pekee.
Bunge linatarajia kuhitimisha kujadili hoja ya hotuba ya mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi za Ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021 kuanzia wiki ijayo ambapo Ofisi ya Waziri mkuu na taasisi zilizo chini yake imeliomba Bunge kuidhinisha Jumla ya Tsh.Bilioni 312,Milioni 802,laki 5 na 20 elfu[312,802,520,000].
Social Plugin