Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WASIOCHUKUA TAHADHARI YA CORONA SONGWE KUTOZWA FAINI


Watu wote ambao hawachukui hatua za tahadhari za kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona kwa kutofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya, watatozwa faini kwakuwa wana hatarisha maisha yao na ya wengine.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa amebainisha hayo jana mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Songwe kufanya ukaguzi wa utayari wa kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona katika Wilaya hiyo.

Opulukwa amesema, “Sasa tunaanza kutoza faini wote wasiofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya kuhusiana na Corona, mfano tukipita dukani au sehemu ya biashara na hakuna maji na sabuni, tuta toza faini na kufunga kwa mda biashara hiyo mpaka mtu huyo azingatie maaelekezo hayo”.

Ameongeza kuwa lengo la Wilaya hiyo ni kuhakikisha kuwa mahali pa kufanyia biashara ni salama kwa wafanyabiashara na watumiaji wa huduma hizo huku akieleza kuwa wanawa fuatilia wageni wote wanao toka nje ya wilaya waliopo katika nyumba za kulala wageni na kuchukua maelezo yao kwa ajili ya tahadhari  endapo wana dalili za Ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Opulukwa ameongeza kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi wote wa Wilaya ya Songwe hususani katika maeneo ya migodi ambapo kuna mikusanyiko ya watu wengi pia ameielekeza kamati inayohusika kutoa elimu ifanye ufuatiliaji wa kina endapo wananchi wanazingatia wanayo waelekeza.

Aidha amesema mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kufanya ukaguzi wa utayari wa Wilaya hiyo katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona, Kamati hiyo imebaini baadhi ya mapungufu ambayo kama wilaya itasimamia kuyarekebisha.

Amefafanua kuwa yote yaliyoonekana kama mapungufu yapo ndani ya uwezo wa Wilaya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha eneo la kuwatenga washukiwa wa Corona lina vitanda vya kutosha na kujenga kichomea taka katika Zahanati ya Saza ambayo itatumika kutibu wagonjwa wa Corona.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe Dkt Humphrey Masoke amesema wameshaagiza vifaa kinga na tiba vyote muhimu katika Bohari kuu ya Dawa ili kuongezea katika vifaa vichache walivyo navyo tayari.

Dkt. Masoke ameongeza kuwa wana endelea kutoa maelekezo na elimu kwa jamii  juu ya tahadhari ya ugonjwa wa Virusi vya Corona kwakuwa bado baadhi ya wananchi wanaamini ugonjwa wa Corona ni wa wazungu hivyo hauwahusu.

Estin Nyangito Mkazi wa Mkwajuni Songwe amesema wamesha pewa elimu ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na Virusi vya Corona na elimu hiyo wataisambaza kwa wananchi wengine ili nao waweze kuchukua tahadhari.

Kwa upande wake Jakson Mwampashi Mkazi wa Songwe amemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kutoa elimu mara kwa mara na kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia magari ya matangazo ya barabarani ili wananchi wote waweze kupata elimu ya Corona


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com