WATUMISHI WA WIZARA YA HABARI WAPEWA MAFUNZO YA KUJIKINGA NA COVID-19

Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamepata mafunzo kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19) katika mazingira yao ya kazini pamoja na maeneo mengine wanayokuwepo. 

Akizungumza na watumishi hao leo katika ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma, Afisa Afya kutoka Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Yusuph Seif amesema kuwa Serikali ipo mstari wa mbele kuhakikisha watumishi na wananchi wanapata elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo ili kuliweka taifa na watu wake katika hali ya usalama dhidi ya ugojnwa huo.

“Virusi hivi ni kabila jipya la virusi vya Corona ambavyo vimegunduliwa mwaka 2019 ambavyo vinasababisha homa kali ya mapafu, kila mtu aendelee kuchukua tahadhari kwa kujikinga na ugonjwa huu” alisema Bw. Yusuph.

Bw. Yusuph ametaja baadhi ya dalili ambazo zinapelekea mtu kushukiwa kuwa ameambukizwa ugonjwa huo ni pamoja na kuwa na homa kali zaidi ya nyuzi joto 38, kukohoa kikohozi kikavu pamoja na mwili kuuma na kuishiwa nguvu.

Ameongeza kuwa ili  kujikinga na ugonjwa huo mtaalamu ni vyema kila mtu awe umbali wa zaidi ya mita moja, kutokusalimiana kwa kushikana mikono, kunawa mikono ipasavyo kwa maji tiririka kwa sabuni ya kutosha yenye kutoa povu jingi angalau kwa zaidi ya sekunde 20 sehemu zote za kiganja cha mkono.

Aidha, amesema kuwa matumizi ya vitakasa mikono (sanitizer) ni njia mojawapo ambayo mtu anaweza kuitumia ili kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni njia sawa na mtu aliyenawa vizuri kwa kutumia maji tiririka na sabuni.

Kuhusu matumizi ya barakoa, Bw. Yusuph amesema kuwa barakoa zinatumiwa na watu wenye dalili za Covid-19, watoa huduma za afya wanapowahudumia wagonjwa ama mtu yeyote anapokuwa kwenye eneo la hatari ya kuwepo au kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Akimkaribisha mtoa mada, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw.Bernard Marceline amewataka watumishi hao kutumia fursa hiyo kujifunza namna ya kujikinga na ugonjwa huo ili waweze kutunza afya zao na wawe wajumbe wa kutunza afya za wengine  pamoja na familia zao ili kuwa salama na hatimaye nchi nzima iwe salama na kujikinga na ugonjwa huo. 

Akishukuru kwa niaba ya watumishi Bw.Johanssen Kaimukirwa ameishukuru Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kazi nzuri wanayoifanya ili watu wote waelewe hatua ambayo itasaidia kujikinga zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post