Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameliomba bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha kiasi cha shilingi Trioni 7.02 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Akiwasilisha hoja hiyo Bungeni jana Jijini Dodoma Mhe Jafo amesema makadirio hayo yanahusisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-(OR-TAMISEMI), Tume ya Utumishi wa waalimu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akifafanua zaidi Mhe Jafo amesema kiasi cha shilingi Trilioni 3.8 kitatumika kwa ajili ya mishahara, Bilioni 851 kwa matumizi mengine na kiasi cha shilingi trilioni 2.29 kitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Serikali imepanga kusimamia utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D by D)
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali itaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikijumuisha utekelezaji wa mpango wa utoaji wa Elimumsingi Bila Ada
Akifafanua zaidi Mhe.Jafo amesema Serikali inampango wa kuratibu ujenzi wa miundombinu ya maeneo ya utawala katika Mikoa, Wilaya, na Halmashauri mpya na za zamani zipatazo 30 ambazo zinatakiwa kuhamia katika maeneo yao ya Utawala
Kuhusu ujenzi wa majengo ya utawala na nyumba za viongozi amesema Serikali itaendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa majengo ya Ofisi na nyumba za makazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi, Maafisa Tarafa na watumishi waandamizi
Hata hivyo amesema itafanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa Kilometa 23,175.11, Makaravati2, 052 na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa 79.9, Ujenzi wa Madaraja 80 yaliyopo vijijini na mijini ili kuimarisha miundombinu ya barabara nchini .
Kwa upande wa Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara Mhe. Jafo amesema Serikali itajenga barabara zenye urefu wa kilometa 35.3 kwa kiwango cha lami na ukarabati urefu wa kilometa 321 kwa kiwango cha changarawe , kukamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 47.59 kwa kiwango cha lami Jiji la Dar-es-salaam.
Wakati Huohuo Mhe. Jafo amesema Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Nzasa-Kilungule-Buza,Ulongoni-Bangulo-Kinyerezi na Magomeni Mapipa- Urafiki na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 11.7 kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni
Mhe. Jafo amesema katika suala la afya Seikali itaendelea kujenga miundombinu ya afya ambapo kutajengwa wodi tatu katika kila Hospitali ya Halmashauri, kuendelea na ujenzi wa Hospitali 27, ujenzi wa Zahanati 3 katika kila Halmashauri na ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali 67 zilizojengwa.
Aidha Mhe. Jafo amesema katika mwaka wa Fedha wa 2020/2021 Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 42.3 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sekondari ambazo zitajengwa katika kila Halmashauri.
Social Plugin