WAZIRI MKUU MAJALIWA: WAGONJWA WAWILI WA CORONA WAMEONGEZEKA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema jana (5 Aprili, 2020) wagonjwa wawili wa corona wameongezeka, hivyo Tanzania ina jumla ya watu 22 waliothibitishwa kuwa na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na kwamba wote wanaendelea vizuri.


Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa waimarishe ulinzi kwenye vituo vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kuwaweka watu wote wanaoingia nchini na wahakikishe hakuna anayetoka ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2020) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Kamati zao za Ulinzi na Usalama za Mikoa ya Mipakani ya Arusha, Rukwa, Katavi, Dar Es Salaam, Tanga, Mtwara, Mara, Pwani, Ruvuma, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Kagera, Kigoma na Songwe.

Waziri Mkuu amesema kati ya wagonjwa hao 12 wapo mkoani Dar Es Salaam, wagonjwa saba wapo Visiwani Zanzibar, Mkoani Kagera kuna mgonjwa mmoja na mkoani Arusha kuna wagonjwa wawili na kwamba Serikali inaendelea kupokea sampuli za vipimo kutoka kwenye mikoa mbalimbali.

“Wagonjwa hawa wote ni wale waliotoka katika nchi mbalimbali, hivyo Wakuu wa Mikoa mnawajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona hususani katika maeneo yanye mikusanyiko.”

Waziri Mkuu amewataka viongozi hao waendelee kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na wahakikishe wageni wote wanaoingia nchini wanapelekwa kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwajili ya kuangaliwa kama wanamaambukizi ya COVID-19.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa wasimamie na wahakikishe watoa huduma katika maeneo hayo wakiwemo walinzi wanapatiwa vifaa kwa ajili ya kujikinga ili wafanye kazi zao bila ya kuwa na mashaka.

“Imarisheni vituo na simamieni watu wasitoke kwenda mitaani na lazima washirikiane ili maambukizi yasizidi kusambaa nchini. Fuatilieni historia za watu wanaoingia nchini kuona maeneo waliyotembelea katika kipindi cha siku 14 kabla ya kuingia nchini.”

Kwa upande wao Wakuu hao wa Mikoa wamesema wanaendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali kuhusu namna ya kukabiliana na virusi vya corona na kuhakikisha havisambai zaidi nchini.

(MWISHO)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post