Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amewaagiza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kuwachukulia hatua wale wote walioanzisha vituo vya mafunzo ya ziada (tuition) wakati ambao shule zote zimefungwa kwa ajili ya kujikinga na corona.
Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kuwataka wanafunzi walioko nyumbani kuacha kuzurura ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
“Wanafunzi watambue kuwa hiyo si likizo bali wamerudi nyumbani kwa sababu ya janga kubwa linaloitesa dunia la virusi vya corona. Kuna baadhi ya sehemu baada ya kusikia watoto wako nyumbani wameanzisha ‘tuition’. Nawataka wote walioanzisha ‘tuition’ waache mara moja,” alionya.
Ndalichako alitoa maelekezo kwa wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa, wasimamie kikamilifu maelekezo ya serikali na kutowafumbia macho watu walioanzisha vituo vya kufundishia kwa sababu wanapingana na maelekezo na wanakuwa tishio la usalama katika maeneo hayo.
Kadhalika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Watoto (Unicef), wametoa angalizo na tahadhari ambazo watoto, wazazi, walezi na walimu wanapaswa kuzichukua wakati wote wa likizo.
“Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, walimu wakuu wasiwaruhusu wanafunzi kukusanyika katika maeneo shule kwa kipindi chote ambacho shule zimefungwa,” tangazo lilielekeza hivyo.
Tahadhari nyingine iliyotolewa, inaitaka jamii iwalinde wanafunzi na watoto wote katika maeneo yao kwa kuhakikisha hawaendi katika maeneo hatarishi yakiwamo yenye msongamano.
Kadhalika wametahadharisha wazazi na walezi wazungumze na watoto wao kuhusu njia za kujikinga na virusi vya corona na kuwasaidia kuendelea kujisomea wakiwa nyumbani.