Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akizungumza na Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamtafuta mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Mwajuma kwa tuhuma ya kumkata na wembe sehemu za korodani ya kulia mme wake aitwaye Shaibu Jabuka (36) mkazi wa mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Aprili 6,2020 majira ya saa saba usiku.
“Shaibu Jabuka alijeruhiwa kwa kukatwa na wembe sehemu za siri korodani ya kulia na mke wake aliyefahamika kwa jina moja la Mwajuma”,amesema Kamanda Magiligimba.
“Chanzo cha tukio hilo ni Mwajuma kunyimwa pesa za matumizi shilingi 10,000/=. Majeruhi amepatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga na kuruhusiwa kutoka”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema jeshi la polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta Mwajuma aliyekimbia baada ya kumkata na wembe mmewe sehemu za siri.
“Natoa wito kwa wananchi wote mkoa wa Shinyanga hususani wanandoa na watu wenye mahusiano ya kimapenzi kuacha kujichulia sheria mkononi pale inapotokea mzozo/mgogoro wasikilizwe wazee wenye busara katika maeneo wanayoishi,wafike ofisi za ustawi wa jamii au Ofisi za Dawati la Jinsia na watoto zilizopo vituo vya polisi ili wasikilizwe kuondoa tofauti zao”,amesema Kamanda huyo wa Polisi.
Social Plugin