Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu wasiojulikana wamemuibia mfanyabiashara Renatus Lucas Maji (44) mkazi wa Mbulu - Kahama shilingi 600,000/= na bunduki yake aina ya Pistol ikiwa na risasi 12 kisha kuitelekeza karibu na eneo la Kituo cha Polisi Kahama.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Aprili 21,2020, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Aprili 20,2020 majira ya saa nne usiku katika hoteli iitwayo Mary's Fast Food Hotel iliyopo mtaa wa Phantom, Tarafa ya Kahama Mjini, Wilaya ya Kahama.
“Renatus Lucas Maji (44),mfanyabiashara, mkazi wa Mbulu - Kahama aliibiwa silaha yake pistol aina ya tisas maker no. T0620-14J00707, car. no. 00108211, cal. 9mm ikiwa na risasi 12 na watu ambao hawajafahamika. Silaha hiyo alikuwa ameifungia kwenye dashboard ndani ya gari lake aina ya toyota clugger no. T.202 DSH alilokuwa ameliacha nje iitwayo Mary's Fast Food Hotel wakati akiwa anakula chakula”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
“Mbinu iliyotumika ni kuvunja kioo kidogo cha abiria upande wa kulia na kuingia ndani ya gari hilo kisha kuiba silaha hiyo pamoja na pesa taslimu Tshs 600,000/= bila yeye mmiliki kujua”,ameongeza Kamanda Magiligimba.
Amesema baada ya tukio hilo msako mkali ukihusisha taarifa za kiintelejensia ulifanyika na kufanikiwa kupatikana kwa silaha hiyo ambayo ilikuwa imetelekezwa karibu na eneo la Kituo cha Polisi Kahama.
Kamanda Magiligimba amesema juhudi za kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa hao zinaendelea na kwamba Renatus Lucas Maji anaendelea kuhojiwa kwa kosa la uzembe kwa kushindwa kutekeleza masharti ya umiliki wa silaha.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wamiliki wa silaha kufuata masharti ya umiliki wa silaha na kwa yeyote atakayekwenda kinyume na masharti hayo atafutiwa umiliki wa silaha mara moja.
Social Plugin