AJALI YA GARI YAUA WATU 6 PWANI


Watu sita wamefariki dunia mkoani Pwani katika ajali iliyoua watu sita.

Ajali hiyo ilitokea  usiku wa kuamkia jana eneo la Vigwaza, Chalinze barabara kuu ya Morogoro na kusababisha vifo vya watu sita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo  akibainisha kuwa tukio la ajali lilihusisha gari lenye namba za usajili T299 AGE aina ya Toyota Prado, lililogongana na gari la mizigo lenye namba za usajili T469 DCP/T 996 BHH aina ya Scania lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara.

Kamanda Wankyo alisema, gari hiyo aina ya Prado ambalo dereva wake bado hajafahamika, lililigonga Scania lililokuwa likiendeshwa na Edger Mbilinyi (30), mkazi wa Njombe.

Alisema, watu waliofariki dunia wote ni wanaume na kati yao yupo mtoto anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 6-7.

Alisema majina yao hayajafahamika na majeruhi mmoja amefahamika kwa jina la Adinani Mresi (30), anayedaiwa kuwa askari wa JWTZ Ngerengere Morogoro aliyeumia sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda Wankyo alisema, chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni dereva wa gari T 299 AGE, Toyota Prado kuendesha kwa mwendo kasi bila kuchukua tahadhari.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani Tumbi na majeruhi anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Mlandizi, huku Jeshi la Polisi likiendelea kumshikilia dereva wa Scania kwa tuhuma za kuegesha gari bila kuchukua tahadhari.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post