Mkuu wa mafunzo na Utendaji Kivita wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Alfred Kapinga amewataka Askari wa jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania JWTZ kuendelea kufanya kazi mama ya Ulinzi wa mipaka na raia kwa nguvu zote.
Meja Jenerali Kapinga alisema hayo wakati akihitimisha mafunzo ya porini kwa kuruti kutoka shule ya mafunzo ya awali ya Kijeshi RTS Kihangaiko kundi la 39 yaliyofanyika kwa siku 14 katika Pori la Pongwe Msungura Bagamoyo Mkoani Pwani.
Meja Jenerali Kapinga aliwataka kuruti hao kujiandaa kufanya kazi ya Ulinzi wa raia kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza jukumu la Msingi litakayoijenga Nchi yetu na kuifanya kukua kiuchumi.
“ Kazi mama ya Jeshi letu ni kulinda mipaka ya nchi na kuwalinda Raia wa Nchi yetu ili waweze kushiriki shughuli za uzalishaji mali kwa Amani na kuletea Taifa Tija inayokusudiwa na kazi hiyo hufanywa na watu imara ambao ni wanajeshi” Alisema Meja Jenerali Kapinga.
Meja Jenerali Kapinga amewasihi kuruti kuendelea kuweka juhudi kwani jeshi lipo imara siku zote na linahitaji watu imara katika kutekeleza majukumu ya kuilinda nchi hivyo mbali na mazoezi walinde Afya zao dhidi ya magonjwa kama Corona na Ukimwi.
Aidha aliwataka wakuu wa Vikosi Jirani na maeneo ya mazoezi kuyadhibiti maeneo hayo kwa namna yeyote yasivamiwe na na Wananchi kwani maeneo hayo ni muhimu kwa ustawi wa jeshi.
“ Hakuna sababu kwa Pori kama hili la Pongwe Msungura Msata kuwaachia raia kwani tumeshawaachia maeneo mengi na katika eneo hili yapo maeneo mengi hakuna sababu ya wao kuingia katika eneo letu la mazoezi ” Alisema Meja Jenerali Kapinga.
Aliongeza kuwa eneo hilo licha ya kuwa halijavamiwa kwa ujenzi lakini wafugaji na wakataji wa miti wachache wameanza kuingia bila kujali kuwa eneo hilo limekuwa likitumika tangu kipindi cha Wagombea Uhuru kwa mazoezi ya Kijeshi.
Aidha amewataka kufanya mazoezi ya mara kwa mara kuepusha Wananchi kuyavamia wakidhani hayana matumizi kwani wakipoteza maeneo hayo hakutakuwa na maeneo mengine.
Aidha alitoa wito kwa raia kutoingia hovyo katika maeneo ya mazoezi ya Kijeshi kwani wanaweza kupatwa na madhara mbalimbali ikiwemo ulipukiwaji wa Mabomu na madahara mengine.
Awali akimkaribisha Mkuu wa shule ya Kihangaiko Kanali Sijaona Myala amesema mafunzo hayo ni moja ya mafunzo ya msingi ya kuwaimarishaAskari katika maisha yao wakiwa jeshini.
Alisema walihakikisha wanajumuisha Vikosi mbali mbali ambavyo humsaidia Askari akiwa Vitani ili kuendelea kuhakikisha tunakuwa na Askari bora wenye Viwango ambao mara zote wamekuwa wakililetea sifa jeshi na Nchi kwa Ujumla.
Pia aliwataka kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Corona kwani hakuna adui mdogo na kwa kufanya hivyo kutawabakisha salama na kuitumikia nchi kikamilifu.
Baadhi ya Askari kuruti Diana Gamanywa na Emanuel Maganga kwa nyakati tofauti wamesema wamejifunza vitu vingi ambavyo vimewaimarisha hasa katika medani ya Vita na kusaidia mamlaka za Kiaraia katika majanga mbalimbali
Katika mazoezi hayo vifaa vya kivita vikiwemo, Ndege, Vifaru,Mizinga na ulipuaji mabomu, pamoja na bunduki za askari vilitumika katika kuonyesha uwezo wao wa mapambano dhidi ya Adui.
Social Plugin