BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU (HESLB) YATOA BILIONI 122.8


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetoa Sh. bilioni 122.8 kwa vyuo na taasisi mbalimbali za elimu nchini kwa ajili ya ada, chakula na malazi ya wanafunzi wanaorejea vyuoni kuendelea na masomo Jumatatu.


Mkurugenzi wa HESLB, Abdul Razaq Badru, aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari.

Alibainisha kuwa, kati ya kiasi hicho, Sh. bilioni 63.7 ni kwa ajili ya chakula na malazi kwa wanafunzi 132,119 kupitia vyuo na taasisi za elimu 81 kwa kipindi cha miezi miwili kwanzia Juni Mosi hadi Julai 30, mwaka huu na kiasi kingine cha fedha ni malipo ya ada.

Alisema malipo ya robo ya nne ambayo ni ya mwisho kwa mwaka huu wa masomo, yatalipwa mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Badru alisema kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita kuanzia Mei 21 hadi Mei 29, mwaka huu, Sh. bilioni 59.1 zilipelekwa vyuoni kwa ajili ya ada za wanafunzi wanufaika ambazo zimelipwa kwa taasisi za elimu ya juu zaidi ya 70 nchini.

“Ni matumaini yetu kuwa fedha hizi zitavisaidia vyuo kutoa huduma bora kwa wateja wetu wapatao 132,119 waliopo katika taasisi za elimu mbalimbali nchini kote," alisema.

Vilevile, alisema tayari bodi imeshapeleka maofisa mikopo vyuoni kwa ajili ya kushughulikia mikopo ya wanafunzi.

Alisema wanafunzi wasiogope kurudi vyuoni kuendelea na masomo kwa sababu serikali imejipanga kwa kila kitu na kuwataka kuanza kuripoti kwa ajili ya kujisajili.

"Ninaomba wanafunzi wasiogope warudi shuleni, ili kuendelea na masomo kama ambavyo imetangazwa na serikali kuanzia Juni Mosi, mwaka huu," alisema.

Alisema usajili wa wanafunzi ulianza juzi na utaendelea hadi kesho, lakini watakaochelewa usajili utaendelea kufanyika Jumatatu.

Badru alisema Benki za biashara ziko tayari kwa ajili ya kusaidia mchakato wa malipo ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post