Na Zena Mohamed, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amekiagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutoruhusu wabunge 15 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuingia maeneo ya Bunge kuanzia jana hadi watakapotimiza masharti mawili waliyopewa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Spika jijini Dodoma leo ilieleza kwamba hatua hiyo ni kwa mujibu we Kanuni ya 144 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayohusu usalama katiko maeneo ya Bunge.
Masharti mawili ambayo wabunge hao wanatakiwa kuyatekeleza ndipo waruhusiwe kuingia bungeni ni pamoja na kurejesha fedha walizolipwa mara moja.
Wabunge hao wanadaiwa kulipwa fedha kwa ajili ya posho sh. 110, lakini hawakuhudhuria vikao vya Bunge kitendo ambacho Spika Ndugai amekifananisha na wizi kama wizi mwingine.
Pili, Spika Ndugai alisema kwa kuwa haijulikani wabunge hao walipo, watalazimika kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizi ya Virusi vya Covid-19 kabla ya kuruhusiwa kuingia Bungeni.
Taarifa hiyo iliwataja wabunge ambao hawatakiwi kuonekana eneo la Bunge kuwa Freeman Mbowe (Kiongozi wa Upinzani Bungeni), Ester Bulaya, Halima Mdee, John Heche, Joseph Mbilinyina Mchungaji Peter Msigwa.
Wabunge wengine ni Rhoda Kunchela, Pascal Haonga, Catherine Nyakao Rage, Devotha Minja, Joyce Mukya, Aida Khenan, Upendo Peneza, Grace Kiwelu na Joseph Haule.
Social Plugin