Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BRELA YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA HALMASHAURI YA MJI MAFINGA


 Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Bi. Saada Mwaruka (kulia) pichani juu wakisaini Mkataba wa makabidhiano ya ya vifaa ya Tehama kwa ajili ya utoaji wa Leseni kimtandao katika Halmashauri hiyo. Makabidhiano hayo yamefanyika jana Mei 19, 2020, katika Ofisi za BRELA Makao Makuu Jijini Dar es salaam.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa (kulia) akimkabidhi Modemu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Bi. Saada Mwaruka (kushoto) kama ishara ya Makabidhiano ya vifaa vya Tehama kwa ajili ya utoaji wa Leseni kimtandao katika Halmashauri hiyo. Makabidhiano hayo yamefanyika leo Mei 19, 2020, katika Ofisi za BRELA Makao Makuu Jijini Dar es salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa amekabidhi vifaa vya Tehama kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Bi. Saada Mwaruka kwa ajili ya utoaji wa Leseni za Biashara kielektroniki katika Halmashauri hiyo.

Makabidhiano hayo yamefanyika jana Mei 19, 2020, katika Ofisi za BRELA Makao Makuu Jijini Dar es salaam yakishuhudiwa na Maofisa kutoka BRELA na Maofisa Biashara kutoka katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga.

Akizungumza katika hafla fupi ya Makabidhiano Bw. Nyaisa ameeleza kuwa lengo kuu la kushirikisha Halmashauri katika zoezi la utoaji Leseni kielektroniki ni kutengeneza mazingira rafiki kwa Wafanyabiashara.

“Mfumo huu ni rahisi sana na unamuwezesha Mfanyabiashara kuweza kupata Leseni akiwa popote pale. Mfumo huu utahitaji Mfanyabiashara aweze kuweka viambatanisho vinavyotakiwa kisha ataweza kupata Leseni yake”. Amebainisha Bw. Nyaisa.

Aidha Mtendaji Mkuu ameeleza kwamba, katika hatua za awali mfumo huu unaweza kuwa na changamoto kadhaa kwa Wafanyabiashara kutokana na matumizi ya mtandao lakini anaamini wakipewa msaada wa karibu basi wataweza kuuzoea mfumo huu mapema.

Amewataka pia kuusimamia vizuri mfumo wa utoaji wa Leseni vizuri ili hata wakati utakapofika wa Halmashauri zingine kuanza kutoa Leseni kuwa mfumo huo basi ziweze kujifunza kutoka kwao.

Vifaa vilivyokabidhiwa siku ya leo ni pamoja na Kompyuta za mezani tatu, Kompyuta mpakato moja, tambaza (scanner) moja, Kichapishi (Printer) moja, Modemu moja na Simu za Mkononi tatu.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Leseni BRELA, Bw. Tawi Kilumile amebainisha kwamba ili mfanya biashara aweze kuomba na kupata Leseni ya Biashara kielektroniki inabidi atembelee tovuti ya www.Business.go.tz kisha kutengeneza akaunti na kuandaa ombi lake la Leseni.
Aidha atatakiwa kuwa na nakala ya Hati ya Usajili wa Kampuni au Cheti cha kuandikisha Jina la Biashara.

Nakala ya Katiba ya Kampuni (Memorandum & Articles of Association) zinazoonesha majina ya wamiliki wa Kampuni , hisa wanazomiliki na saini zao.

Nakala ya Hati ya kuandikishwa kama mlipa kodi (TIN), nakala ya Mkataba wa pango, nakala za Vitambulisho vya wenye hisa katika Kampuni.

Kibali/Hati/Leseni kutoka kwenye Mamlaka za Udhibiti kwa biashara zinazodhibitiwa na Mamlaka za Serikali (Wizara, Mamlaka, Idara, Taasisi au Wakala za Serikali) cha kuruhusu kufanyika kwa biashara husika.

Vigezo hivyo vikiwa ni kwa Leseni itakayomilikiwa na Kampuni au Mtu/Watu wenye kumiliki Jina la Biashara.

Na ikiwa Mwenye biashara ni Mtu Binafsi basi atatakiwa kuwa na nakala za Kitambulisho cha mwenye Biashara kama vile Pasi  ya kusafiria, Kitambulisho cha Taifa, Kitambulisho cha Mpiga kura au Cheti cha kuzaliwa (kwa raia wa Tanzania), na kibali cha Kuishi Nchini kwa asiye Mtanzania.

Nakala ya Hati ya kuandikishwa kama mlipa kodi (TIN).
Nakala ya Mkataba wa pango au Hati ya Umiliki yenye  jina lake. Nyaraka hizi ni kwa ajili ya uthibitisho wa mahali biashara husika itakapokuwa inafanyika

Akitoa shukrani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga ameishukuru BRELA kwa kuwapatia vifaa hivyo na kuahidi kuvitumia kama ilivyo kusudiwa ili kuweza kutimiza lengo la Serikali la kufikia uchumi wa Kati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com