China imetangaza kulipiza kisasi kama Marekani itajiingiza katika masuala ya nchi yake hasa eneo lake la Hong Kong baada ya nchi hiyo kuionya kuwa itaiwekea vikwazo kutokana na mswada wa sheria kuhusu usalama huko Hong Kong.
Zhao Lijian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Uchina, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba China itachukua hatua za kulipiza kisasi ikiwa Marekani itaendelea kuathiri masilahi yake huko Hong Kong.
Zhao Lijian amesema Marekani inajaribu kuhatarisha usalama wa kitaifa wa China. Ameongeza kuwa Beijing imewasilisha barua kwa utawala wa Marekani dhidi ya kauli ililiyotolewa hapo awali na mshauri wa usalama wa taifa katika ikulu ya White House Robert O'Brien.
Jumapili Mei 24, Robert O'Brien alisema kwamba sheria mpya iliyopendekezwa na China inaweza kusababisha Marekani inaiwekea vikwazo nchi hiyo na kutishia kukata msaada wa kifedha kwa kituo cha kifedha cha Hong Kong.
Wakati huo huo China imesema uhusiano baina yake na Marekani unakaribia kiwango cha enzi mpya ya vita baridi, inayochochewa na mvutano kuhusu janga la virusi vya corona, miongoni mwa mengine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema jana kuwa Marekani imepatwa na virusi vya kisiasa vya kufanya mashambulizi mfululizo dhidi ya China, na kusisitiza kuwa licha ya hayo, Beijing itaendelea kuunga mkono juhudi za kimataifa za kulitafutia suluhu janga la Corona. Rais wa Marekani Donald Trump anaituhumu China kuficha ukweli juu ya mripuko wa virusi vya corona, na anaeneza nadharia ya kwamba virusi hivyo viliponyoka kutoka maabara ya siri ya nchini China.