Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA EYP LAUNGANA NA SHIRIKA LA SEMA KUTOA ELIMU YA CORONA

Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Empower Youth Prosperity (EYP) lenye makao yake makuu Jijini Mbeya na Sustanable Environment Management Action (SEMA) la Mkoani Singida yameunganisha nguvu katika kutoa elimu ya kujikinga na Maambukizi ya Virusi corona  kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kutoa Elimu hiyo Mei 11,2020 kwenye eneo la Soko Kuu la Manispaa ya Singida Ofisa Mradi kutoka Shirika la SEMA Renard Mwasambili amesema programu wanayoitekeleza ni utoaji Elimu ya namna ya unawaji Mikono, utoaji wa Vifaa sambamba na elimu ya utengenezaji wa vifaa vya kujikinga na Virusi vya Covid 19 vinavyosababisha Ugonjwa wa Corona.

“Lengo la Elimu hii ambayo tunaifanya ni kutembelea maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu na kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja,makundi na wafanyabiashara namna ya kujikinga dhidi ya Ugonjwa huu”,alisema Mwasambili.

Alisema  programu hiyo imewashirikisha pia maafisa wa Shirika la Empower Youth Prosperity (EYP) kutoka mkoani Mbeya na kuongeza kuwa Kila mtanzania mahali alipo anapaswa kuchukua tahadhari na kamwe asipuuze ushauri wa kitaalamu unaoendelea kutolewa na Serikali pamoja na wataalamu wa afya.

Mkurugenzi wa Shirika la Empower Youth Prosperity (EYP) Mwakyusa amesema wanaendelea kutoa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona ambao umekuwa tishio nchini na duniani kote huku akibainisha lengo la Umoja wao ni kupanua mahusiano yao na kuhakikisha ugonjwa Corona unatokomezwa.

Shirika la EYP lilianza mapambano haya mwanzoni mwa mwezi Aprili mkoani Mbeya na mkoa wa Songwe.

Kwa mujibu wa Afisa wa elimu ya afya kwa jamii na mkuu wa kitengo cha tafiti cha Empower Youth Prosperity (EYP) Ndg Amani Twaha amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kutoa elimu kwa zaidi ya watanzania 21,520 katika mkoa wa Sngida na Mbeya na kwamba elimu hiyo inatolewa pia katika mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook, Instagram na Whatsapp.

Amani amesema wanatarajia kutoa elimu hiyo katika mikoa mingine ya Tanzania ikiwa ni pamoja na mkoa wa Songwe unaotarajiwa kufikiwa hivi karibuni.


Mwezeshaji wa Mradi kutoka shirika la SEMA, Witness Anderson alisema homa kali ya mapafu inayosababisha Virusi vya Corona ni Ugonjwa unaoambukizwa kwa kuingiwa na maji maji yatokayo kwenye njia ya hewa wakati mtu mwenye Ugonjwa huo anapokohoa ama kupiga chafya.

Alitaja njia nyingine ya maambukizi ni kwa kugusa maji maji yanayotoka puani (kamasi),kugusa kitambaa au nguo zilizotumiwa na mtu mwenye maambukizi ya Ugonjwa huo au maeneo mengine yaliyoguswa na mtu mwenye Virusi vya Corona.

Akielezea jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo alitoa tahadhari ya watu kukaa mbali angalau mita moja au mbili jambo litakalosaidia kujiepusha na maambukizi iwapo mmoja kati ya watu hao atakuwa na maambukizi.

Alisema tahadhari nyingine inayopaswa kuchukuliwa ni kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kutumia kitambaa safi au sehemu ya mbele ya kiwiko cha mkono,kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo, kusalimiana kwa kushikana mikono,kukumbatia na kubusiana.

“Safisha mikono yako mara kwa mara kwa maji tiririka kwa kutumia sabuni au dawa ya kutakasa mikono na baada ya kunawa epuka kugusa macho,pua au mdomo na nguo badala yake jifute kwa kutumia tishu ambayo itatupwa sehemu salama baada ya kutumika”,alisema Anderson.

Baadhi ya maeneo ambayo shirika EYP na SEMA walitoa elimu hiyo mkoani Singida ni pamoja na eneo la Soko Kuu la Manispaa ya Singida, Soko Kuu la kimataifa la Vitunguu, Kituo kikuu cha mabasi,vituo vya bajaji, bodaboda, vituo vya kuuza mafuta, mama lishe, barabarani ambapo pia kwa siku ya leo May 12 watakwenda kutoa elimu hiyo katika wilaya za Iramba, Manyoni, Ikungi, Singida DC.
Afisa wa Shirika lisilo la Kiserikali la Sustanable Environment Management Action (SEMA) la Mkoa wa Singida, Witness Andersoon (kushoto) akitoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara wa Soko la Vitunguu la Kimataifa la Manispaa ya Singida namna ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona mkoani Singida
Mmoja wa maafisa wa shirika la EYP Amani Twaha akiendelea kuota elimu kwa wakina mama mkoani Singida
Vita hii dawa yake ni elimu kwa kila kundi
Baadhi ya maafisa wa SEMA na EYP waliojitoa kuoa elimu juu ya ugonjwa wa corona
Elimu ikitolewa kwa madereva barabarani.
Baadhi ya mabango yaliyotumika kufikisha ujumbe
Maafisa wa Shirika hilo, wakitoa elimu kwa njia ya mabango.
Elimu ikitolewa Stendi Kuu ya Mabasi.
Msafiri akitoa maoni yake kwa mwanahabari kuhusu ugonjwa wa Corona.
Elimu ikitolewa kwa Mama Lishe.
Elimu ikitolewa katika vituo vya kuuza mafuta.
Elimu ikitolewa kwa madereva barabarani.
Elimu ikitolewa kwa madereva wa Bajaj.

JUA ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA CORONA

Virusi vya Corona (Cov) ni familia ya virusi vinavoysababisha ugonjwa kuanzia mafua ya kawaida hadi magonjwa makali zaidi kama vile matatizo ya kupumua (MERS-CoV) na SARS-CoV.

Virusi vya Corona vya COVID-19 ni mripuko mpya uliogunduliwa mwaka 2019 na havikuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa bindamu. Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi, shida katika kupumua, na katika hali ngumu zaidi, maambukizi yanaweza kusababisha, nimonia, kukosa pumzi, kushindwa kufanyakazi kwa figo na hata kifo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com