FRANKFURT, Zaidi ya watu 40 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona (COVID-19) baada ya kuhudhuria ibada kanisani katika mji wa Frankfurt nchini Ujerumani hii ikiwa ni kwa mujibu wa Idara ya Afya katika mji huo.
Ili kuzuia maambukizi zaidi, mamlaka yamji huo wa Hanau imefutilia mbali hafla nyingine iliyopangwa kufanyika mjini humo.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametetea vikwazo vilivyowekwa na serikali yake kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona. Mwanasiasa huyo wa kihafidhina amesema, anaelewa ni kwa nini kumekuwepo na ukosoaji kuhusu vikwazo hivyo.
Kansela Merkel aliongeza kuwa, ilikuwa ni muhimu kuwekwa vikwazo hivyo ili kulinda haki za msingi wa raia ikiwemo afya.
Amesema, amefurahishwa na jinsi hali ilivyo sasa kwani imewezesha kufungua mwanya wa kufunguliwa tena shughuli za kiuchumi ambazo zilikuwa zimepigwa marufuku kutokana na janga la virusi vya Corona.
Kansela huyo wa Ujerumani amesema, janga la ugonjwa wa Covid-19 limekuwa changamoto kwa jamii, ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kuikabili Ujerumani katika muda wa miaka 71 tangu kupitishwa katiba ya Ujerumani mnamo Mei 23, mwaka 1949.
Aidha, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Amerika ya Kusini ndio kitovu kipya cha mlipuko wa virusi vya Corona. Hiyo ni baada ya takwimu kuonyesha kuna kasi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo katika eneo la Marekani ya Kusini na Kati. Watu wapatao milioni 5.2 wameambukizwa na wengine 337,000 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid- 19.
Aidha, nchini Brazil, idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Covid-19 imefikia 20,000 kwa sasa na watu 310,000 wameambukizwa.
Brazil sasa ni nchi ya tatu yenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa baada ya Marekani na Urusi. Wakati maambukizi yakiendelea kuongezeka kwa kasi kubwa Amerika ya Kusini, nchi za Bara la Ulaya na Marekani zinaendelea kupata afueni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez amesema nchi hiyo haitafungua mipaka yake ili kuruhusu watalii hadi mwezi Julai, mwaka huu.
Tangazo la Waziri Mkuu huyo limeondoa uwezekano wa kurudi kwa shughuli za kitalii katika taifa hilo ambalo ni miongoni mwa mataifa yalioathirika zaidi na janga la virusi vya Corona barani Ulaya.
Italia ambayo ni nchi nyingine iliyoathirika na ugonjwa wa Covid-19 barani Ulaya, imetangaza kufungua mipaka yake kwa watalii kuanzia Juni 3, mwaka huu.
Mbali na hayo, wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana wameshiriki katika sala ya Idul Fitr baada ya kukamilisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Ofisi ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilitoa taarifa na kusema, jani ni tarehe Mosi Shawwal na siku kuu ya Idul Fitr.
Kwa mujibu wa maamuzi ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na COVID-19, kulikuwa na idhini ya kuswali sala ya Idul Fitr katika miji yote.
Hata hivyo, kwa mujibu wa maelekezo ya idara hiyo hakukuwa na sala katika viwanja vikubwa bali watu walijimuika makundi madogo madogo katika misikiti na viwanja au bustani mitaani ambapo waumini walioshiriki katika sala walizingatia kanuni ya kutokaribiana na kuvaa barakoa.
Kwa kawaida sala ya Idi huswaliwa mjini Tehran katika Uwanja wa Swala wa Imam Khomeini ambao una uwezo wa kubeba maelfu ya watu, lakini mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 wakuu wa afya nchini Iran walishauri kuwa waumini wasijumuike katika eneo hilo.