Halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga imetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa baraza la waislam Tanzania (BAKWATA) wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.3 kwa waumini wa dini ya kiislam wilayani Kahama ambao utatumika katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akikabidhi msaada huo leo kwa Shekhe wa wilaya ya Kahama, Alhaj Omary Damka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Anderson Msumba amesema msaada huo unalenga kuwauga mkono waumini hao katika mwezi huu maalumu wa toba.
“Halmashauri ya Mji kahama imetoa Michele, kg 1000, unga wa ngano kg 100, Sukari Kg 200, mafuta ya kula Lita 200, Maharage kg 442 na tambi boksi 40,tunaomba msaada wetu upokelewe,sisi tumetoa kiasi hiki kidogo tunaimani kitawasaidia,”alisema Msumba.
Msumba aliongeza kuwa Halmashauri inatambua mchango wa viongozi wa dini na itaendelea kushirikiana nao katika Nyanja mabalimbali ili kuhakikisha jamii inakuwa na hofu ya Mungu na kutenda matendo Mema.
“Viongozi wa dini tunathamini uwepo wao hasa katika kipindi hiki cha Janga la Ugonjwa wa Covid 19 wamekuwa mstari wa mbele kwa kuiombea Halmashauri yetu na taifa kwa Ujumla ambapo waumini katika nyumba za ibada wanaendelea kuhimizwa kuhusiana na namna ya kuchukua tahadhari,”alisema Msumba.
Akipokea Msaada huo Shekhe wa wilaya ya Kahama Alhaj Omary Damka ameishukuru Halmashauri ya Mji kahama kwa msaada huo ambao umekuja katika kipindi muhimu cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo kuna wahitaji wengi katika jamii hususani kundi la wazee wasiojiweza na watoto yatima.
“Msaada huu tutawapatia watoto yatima,Wazee wasiojiweza sambamba na wahitaji wengine tunawashukuru kwa moyo wenu mzuri wa kutushika mkono katika kipindi hiki cha toba hakika mmefanya jambo jema la kumpenda Mwenyezi Mungu,”alisema Damka.
Sambamba na hilo Damka amewataka waumini wa kiislamu kuendelea kuchukua tadhari dhidi ya Ugonjwa wa Covid 19 kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kunawa mikono na sabuni,kuvaa barakoa na kutokwenda kwenye mikusanyiko isiyokuwa na tija.
Mwisho.