Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LHRC WACHANGIA VIFAA KINGA, MAPAMBANO DHIDI YA CORONA

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (katikati) akiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume wakati wa makabidhiano ya vifaa kinga.
***

Katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya namna ya kukabiliana na maambukizi. 

Maambukizi ya virusi vya corona yanaathiri haki za msingi ikiwemo haki ya kuishi, haki ya kufanya kazi na kupata ujira, haki ya kujumuika na hata haki ya kuishi, hii inailazimu LHRC kutoa elimu kwa jamii kwa ujumla na makundi yanayoathirika zaidi kufuatia mlipuko wa COVID-19. 

Sambamba na kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa makundi haya, LHRC imeendelea kushirikiana na wadau na mamlaka za serikali ikiwemo Wizara ya Afya katika kukabiliana janga hili.

 Leo Mei 11, 2020, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimechangia kwa serikali vifaa tiba ikiwemo mavazi ya kujikinga (PPE) 300 na barakoa za madaktari 300 vyenye jumla ya thamani ya milioni 21. 

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyia jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga amesema LHRC kama watetezi wa haki za binadamu wameguswa na janga la corona na wameamua kuchangia sekta ya afya kwa kuzingatia kwamba sekta hiyo iko mstari wa mbele katika kukabiliana na virusi vya corona. 

“Tumeguswa kuchangia kidogo tulichojaaliwa na tukaona tuchangie vifaa vitakavyowasaidia watoa huduma za afya kuendelea kutoa huduma huku wakilinda haki yao ya afya. LHRC tunafanya utetezi wa haki zote za binadamu na katika hili la haki ya afya tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua kukabiliana na corona” – alisema Anna Henga 

Kwa upande wake mwakilishi wa Serikali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume amewashukuru LHRC kwa kutoa vifaa hivyo na kuwataka wadau wengine kuendelea kutoa misaada kwa sekta ya afya.‬

‪“Huu ni msaada tuliokuwa tunauhitaji sana, tunafahamu vifaa hivi vina gharama kubwa lakini ninyi mmejitoa kwa kujali umuhimu wa haki ya afya. Tunawashukuru kwa kujitoa na tunawakaribisha wadau wengine wachangie zaidi”. alisema Dkt. Mfaume‬

Katika mapambano dhidi ya virusi vya corona wadau mbalimbai wameungana na serikali kwa namna mbalimbali kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa huo hatari nchini. LHRC wanakuwa sehemu ya wadau waliochangia katika utoaji elimu na utoaji wa misaada ya moja kwa moja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com