Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WATOA MISAADA YA KIBINADAMU KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO YA ONGEZEKO LA KINA CHA MAJI ZIWA TANGANYIKA


Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilali Muslim Tanzania Mohsin Abdallah Sheni (wa pili kushoto) akikabidhi kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Emanuel Maganga (katikati mwenye kofia) sehemu ya shehena ya tani 2.5 ya aina mbalimbali za vyakula zilizotolewa kwa waathirika wa mafuriko katika vijiji 14 vya wilaya ya Uvinza ambapo kiongozi huyo pia alichangia mifuko 100 ya saruji.


Na Moureen Tesha - Kigoma
Wadau wa Maendeleo ikiwemo Taasisi ya Bilali Muslim Tanzania na Red Cross Tanzania wametoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi 116 walioathiriwa na mafuriko kufuatia kuongezeka kwa kina cha maji ya ziwa Tanganyika na maji hayo kuzingira nyumba zao na hivyo kulazimika kuhama makazi yao.


Wahanga hao wamepatiwa misaada hiyo mbele ya Mkuu wa mkoa kigoma,Emmanuel Maganga katika kijiji cha Ilagala ambapo Mkuu wa wilaya Uvinza Mwanamvua Mrindoko alisema kuwa jumla  ya kaya 311 katika vijiji 14 vya kata sita za Halmashauri ya wilaya Uvinza mkoani Kigoma zimeathirika na mafuriko hayo.

Pamoja na kuathirika kwa makazi ya watu lakini pia maji hayo yameathiri miundo mbinu ya barabara kwa baadhi ya mito iliyokuwa ikiingia kwenye ziwa Tanganyika ambayo maji yamekuwa yakitoka ziwani na kurudi barabarani na hivyo kuharibu daraja la mto Lagosa na sehemu kubwa ya barabara ya Ilagala kwenda Kalya kuathiriwa na maji hayo.


Mrindiko aliitaja misaada  hiyo ambayo imetolewa na wahisani mbalimbali wakiwemo Red Cross Tanzania waliotoa magodoro 100, blanketi 200, ndoo za kuchotea maji 100 na madumu ya kuhifadhia maji 100 huku  ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma ilichangia kiasi cha shilingi milioni 2.5.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataja wengine waliochangia kwenye misaada hiyo ni pamoja na Taasisi ya Bilali Muslim Tanzania ikiwakilishwa na Mwenyekiti wake, Mohsin Abdallah Sheni ambao walitoa tani 2.5 za chakula cha aina mbalimbali ikiwemo mifuko 100 ya sukari na  mifuko 100 ya saruji huku Kigoma Hiltop ikitoa mifuko 40 ya unga wa sembe.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa walengwa Mkuu wa mkoa Kigoma, Emanuel Maganga aliwapa pole watu wote walioathirika na mafuriko hayo na kusema kuwa msaada huo ni kutoa faraja kwa waathirika na siyo kukidhi mahitaji yao  huku akitoa wito watu wote kuhama mabondeni na kwenye mkondo wa maji kabla madhira makubwa zaidi hayajatokea.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Hadija Kayanda mkazi wa Kijiji cha Ilagala wilaya ya Uvinza alisema kuwa wameishi kwenye maeneo hayo kwa muda mrefu lakini wameshingazwa na namna maji yalivyojaa ziwani na kufikia kwenye maeneo yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com