MASHAURI 4,711 YASIKILIZWA KWA MAHAKAMA MTANDAO KUEPUKA CORONA


Na Magreth Kinabo –Mahakama     
Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kuendesha mashauri 4,711 kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video Conference’ ikiwa ni hatua mojawapo  za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 1 9 katika kipindi cha miezi miwili.


Mashauri  hayo yamesikilizwa kwa njia  hiyo, kufuatia  utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa  Tanzania, Prof. Ibrahim  Hamis Juma alilolitoa Machi 23, mwaka huu la kutumia  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwaepusha Watumishi wa Mahakama, Magereza, wafungwa na mahabusu na wateja wengine wa Mahakama dhidi ya maambukizo hayo, wakati shughuli za utoaji haki zikiendelea kufanyika.

Agizo hilo lilitolewa na Prof. Juma kupitia mkutano wake na waandishi wa  habari uliofanyika Jijini Mwanza, la kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye kipindi hichi ambacho Tanzania na dunia kwa ujumla  kukumbwa  na janga la ugonjwa huo.

Akizungumzia kuhusu usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Machumu Essaba alisema imelipunguzia pia Jeshi  la Magereza gharama za usafiri wa kila siku za kuwaleta wafungwa au mahabusu mahakamani na msongamano.

‘‘Njia hii imetumika katika kipindi cha ugonjwa huu, kuanzia Machi 23, mwaka huu  hadi Mei 26, mwaka huu, ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania, imesikiliza mashauri 48 kupitia vikao vitano, kati ya hivyo vitatu vilifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, vilivyohusisha mashauri 30 na kimoja Tabora kilichohusisha mashauri tisa na kingine Iringa kilichokuwa na mashauri tisa,’’ alisema Essaba.

Alisema  kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza mashauri 3,188 kati ya hayo, mashauri 804 ymesikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama za Wilaya, Kinondoni 714, Ilala 992, Temeke 523, na  Kigamboni 155.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mahakama ya Mkoa na Wilaya mashauri yaliyosikilizwa kwa teknolojia hiyo ni 367,  kanda  zingine ni Tanga 310, Musoma 158, Tabora 130, Dodoma 78, Mtwara 66, Moshi 46, Arusha 41, Kigoma, 37,  Sumbawanga 23,  Iringa 15, Songea 14, Shinyanga 12, Mwanza 28 na Bukoba 5.

Essaba  alifafanua kwamba Mahakama Kuu Divisheni za Biashara imesikiliza mashauri 55 na Kazi mashauri 90, ambazo zilitumia vifaa vilivyopo kwenye maeneo yao.

Aidha  aliongeza kwamba  zaidi mashauri 300 yamesikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kutumia simu ya mezani ‘Teleconference’ kwa sababu kuna tatizo la ukosefu wa huduma ya  mtandao ‘internet’ kwenye ofisi  za Mwanasheria  wa Serikali, hali inayosababisha kutumia njia hiyo.

Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na Virusi vya Corona ulikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu yaTanzania Aprili 16 mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kusikiliza mashauri kwa  teknolojia hiyo,

Awali teknolijia hiyo  ilikuwa inatumika katika vituo sita, ambavyo ni mfumo huo, umefungwa ambavyo ni  Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda za Dar es salaam, Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post