Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KHAMIS MGEJA AGEUKIA KILIMO CHA MPUNGA BAADA YA KUPUMZIKA SIASA


 Khamis Mgeja akimsaidia Salma Kazinza mkazi wa Nyanhembe kusukuma baiskeli iliyobeba mpunga kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara. 
 Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis Mgeja akiwa ameshikilia  mpunga uliokatwa katika shamba lake la Nyanhembe Kata ya Kilago wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis Mgeja  akiwa katika harakati za kupiga mpunga

Na Paul Kayanda,Kahama
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis Mgeja inayojishughulisha na shughuli za Kilimo na Ufugaji, ameipongeza serikali kupitia wizara ya kilimo kutokana na kuliagiza shirika la kuhifadhi chakula NFRA kununua mazao mbalimbali ya wakulima badala ya kununua mahindi pekee.

Mgeja ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga(CCM) amesema uamuzi huo utatenda haki kwa wakulima wote wanaojituma katika kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara tofauti na kipindi kilichopita.

Ametoa pongezi hizo baada ya kutembelewa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari katika shamba lake la mpunga, lililopo Kijiji cha Nyanhembe Kata ya Kilago wilayani Kahama.

Mgeja amesema wakulima wamemsikia na kumuona hivi karibuni Waziri wa kilimo Japhet Hasunga akiwa Mkoani Manyara akitoa maelekezo kwa NFRA kununua mazao yote yanayolimwa na wakulima likiwamo zao la mpunga.

Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm alisema uamuzi huo wa serikali utakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri katika mazao yao pamoja na wafanyabiashara wanaonunua mazao kutoa bei nzuri.

Amesema katika msimu huu amelima ekari 73 ambapo anatarajia kupata mavuno ya gunia za mpunga 1430,  ambapo mpaka sasa tayari amevuna magunia 320 huku akitaja lengo lake kuu katika msimu ujao ni kulima ekari 250.

Hata hivyo Mgeja amedai kuwa kwa sasa ameamua kupumzika siasa na kubainisha kwamba kwa sasa amejielekeza katika kilimo na ufugaji wa ng’ombe,mbuzi na ufugaji wa nyuki pamoja na samaki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com