MKEMIA FIDELIS SEGUMBA ATOA USHAHIDI KESI YA SHAMIM MWASHA NA MUMEWE


Mkemia, Fidelis Segumba amedai mahakamani kwamba katika bahasha tano alizochunguza katika kesi ya Shamim Mwasha na mumewe, mbili zimebainika kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroine.


Segumba ambaye ni mkemia daraja la kwanza na shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai hayo jana Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Elinaza Luvanda, wakati akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula.

Mstakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Abdul Nsembo ambapo wanadaiwa Mei mosi mwaka 2019 walikutwa na dawa za kulevya nyumbani maeneo ya Mbezi Beach.

Jana Segumba akitoa ushahidi wake alidai alikabidhiwa bahasha tano na ofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Suleiman Juma Mei 2 mwaka jana.

Alidai bahasha hizo zilipewa majina A ikiwa na gramu za unga 232.70, B unga gramu 68.52, C gramu 8.27, D gramu 42.70 na E gramu 7.

Anadai katika uchunguzi alibaini bahasha A na D zilikuwa na unga wa dawa za kulevya aina ya heroine wakati bahasha zingine tatu hazikuwa na dawa za kulevya.

Alidai, heroin husababisha ulevi usioponeka kirahisi, ulemavu wa akili na ipo katika orodha ya kwanza ya dawa zenye sumu.

“Bahasha A kulikuwa na unga uliofungwa kwenye kitambaa cheupe kilichofungwa na nailoni angavu ndani kulikuwa na unga mweupe, bahasha B hadi E ndani kulikuwa na kikopo kilichokuwa na unga, baada ya kusajili bahasaha hizo ndipo nilipoanza uchunguzi,”alidai.

Alidai baada ya kumaliza uchunguzi aliandika ripoti na kuisaini ambapo aliiomba mahakama iipokee ripoti hiyo kama kielelezo.

Hata hivyo mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo kwa madai kuwa shahidi hakufata sheria ya kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani kwani ripoti hiyo haikuwa chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali bali alipewaa mwendesha mashtaka mahakamani.

Mawakili hao ni Juma Nassoro, Josephat Mabula na Hajra  Mungula.

Akijibu Wakili Kakula alidai hoja hizo zimewasilishwa mapema kabla ya muda, walipaswa kusubiri hadi shahidi wa mwisho hivyo alidai hazina mashiko zitupwe.

Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na kupokea ripoti hiyo kama kielelezo namba moja baada ya kukubaliana na hoja za upande wa mashtaka kwamba hoja ziliwasilishwa mapema kabla ya muda wake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post