Na Ahmed Mahmoud,,Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema ataishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa utaratibu wa sasa wa kuwaweka kwenye karantini ya siku 14 wageni wote wanaoingia mkoani hapa kwa shughuli za utalii ili kuepusha kuwakatisha tamaa.
Gambo amelazimika kutoa kauli hiyo mapema leo wakati akipokea msaada wa Lita 500 za vitakasa mikono kutoka kampuni ya bia nchini, TBL na kueleza kwamba njia sahihi ya kuendelea kuchapa kazi ni pamoja na kuruhusu watalii walioonyesha nia kuingia nchini kama njia moja wapo ya kuvutia utalii .
Alisema wapo wageni wengi walioonyesha nia ya kutembelea vivutio mbalimbali mkoani hapa ila wanakumbwa na kikwazo cha Karantini jambo linalowakatisha tamaa na hivyo ameonelea ipo haja ya kuishauri serikali kubadilisha kipengere hicho ili kuangalia namna nzuri zaidi itakayowapendeza watalii bila kueneza maambukizo ya Korona.
Amesema sekta ya utalii ni muhimu sana kwa ustawi wa mkoa wa Arusha hivyo ameonelea ipo haja kwa watalii walioonyesha nia yakuingia nchini kuanzia mwezi juni mwaka huu kupewa utaratibu mpya wa maambukizi ya ugonjwa wa Korona badala ya kuwekwa kwenye Karantini ambayo huwapotezea muda na kuwaongezea gharama zaidi.
“Tunafikiria mkoa wa Arusha kuishauri serikali ili kile kipengere cha Karantini iweze kukiondoa ili kuepuka kuwakatisha tamaa watalii walioonyesha nia ya kuja mkoani hapa kuanzia mwezi juni mwaka huu”Amesema Gambo
Katika hatua nyingine Gambo alisema kuwa mkoa wa Arusha utaendelea kutoa elimu kwa wananchi sanjari na kuwaondoa hofu ikiwemo kuondoa misongamano isiyo ya lazima kwa kuweka utaratibu wa mazishi kwa watu wasiozidi 10 na kuwa sio kila anayefariki basi amefariki wa Ugonjwa wa Covid 19.
Awali Meneja Uzalishaji wa kiwanda Cha bia cha TBL ,Joseph Mwaikasu alisema kampuni imeona uhitaji wa jamii na kuunga Juhudi za Serikali za kukabiliana na Ugonjwa wa homa Kali ya mapafu Covid 19 kwani hata wafanyakazi wao idadi kubwa ni wakazi wa mkoa wa Arusha.
Alisema kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha waendelea kusaidia katikamapambano dhidi ya janga hili hatari
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Richard Kwitega alizipongeza baadhi ya Taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa yakitoa vifaa kwa ajili ya kupambana na Ugonjwa huo na kutaka wengine kuendelea kujitokeza kusaidia.
Social Plugin