Na,Amiri Kilagalila,Njombe
Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Charles Mwinami (45) mkazi wa kijiji cha Itunduma wilayani Njombe amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumwingilia kimapenzi mjukuu wake mwenye umri wa miaka 5 na kutakiwa kulipa fidia ya shilingi Milioni Kumi kwa mwathirika.
Akisoma kesi no 12 ya 2020 hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoani Njombe Hassan Makube amesema mtuhumiwa amekutwa na hatia hiyo baada ya ushahidi wa daktari kuthibitisha mwathirika alifanyiwa kitendo hicho.
Mama mzazi wa mtoto huyo ameiambia mahakama kuwa wakati mtoto wake akifanyiwa ukatili huo alikuwa nje ya mkoa akifanya kazi za vibarua.
Shahidi namba nne ambae ni mtendaji wa kijiji cha Itunduma ameieleza Mahakama kuwa alipopata taarifa za tukio hilo alimwita mtoto ofisini kwake na kumhoji ambapo alikiri kulala na babu yake kitanda kimoja na kufanyiwa ukatili huo.
Mtoto huyo amekiri pia mbele ya mahakama kuwa alikuwa akilala na babu yake kitanda kimoja na kufanyiwa ukatili huo mara zote tangu mama yake kusafiri.
Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na kujiridhisha mahakama imeona mshitakiwa Charles Mwinami anakosa la kujibu ambapo alipopewa nafasi ya kujitetea alikana kufanya kosa hilo huku akisisitiza kuwa wakati huo hakuwa na ndugu wa kumwachia mtoto huyo kulala nae.
Jopo la mawakili wa serikali likiongozwa na Hendry Mandwa na Happness Makungu wameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
Akisoma hukumu hiyo hakimu Mkazi Mfawidhi Hassan Makube amesema kwa mujibu wa kifungu cha sheria no 158 kifungu kidogo cha kwanza A sura ya 16 mshitakiwa amekutwa na kosa hivyo amehukumiwa kwenda jela miaka thelathini na kutakiwa kulipa fidia ya shilingi Milioni Kumi kwa mwathirika.
Hata hivyo hakimu Makube amesema mahakama imeona kosa lingine la kubaka lakini hajatoa adhabu yake kwa sababu halikuwa kosa aliloshitakiwa nalo mtuhumiwa huyo.
Social Plugin