Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dr. Evamarie Semakafu, ametembelea Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, kukagua maandalizi ya kuwapokea wanafunzi tarehe 01 Juni 2020, kufuatia tamko la hivi karibuni la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli la kufungua Vyuo Vikuu nchini, baada ya kuvifunga kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na virusi vya Corona.
Aidha, amekagua maandalizi ya ratiba ya masomo, usajili wa wanafunzi unaoendelea, utekelezaji wa agizo la Wizara la kufanya malipo kwa wakati kwa wanafunzi wa mikopo ya Elimu ya Juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo Tanzania, pamoja na hatua za tahadhari ambazo Chuo imezichukua hadi sasa kuwakinga wanafunzi na maambuziki ya Corona.
Ameridhishwa na hali katika Kituo cha Afya kinachotoa huduma, ufungaji wa vifaa vya kunawa mikono kabla ya wanafunzi kuingia madarasani, pamoja na elimu ya jumla inayohusu tahadhari binafsi kwa wanafunzi.
Prof. Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo; amemhakikishia Naibu huyo utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kadhalika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto na kwamba kwa zaidi ya asilimia 98% maandalizi yote msingi yamekamilika na tayari wanafunzi wameshaanza kuingia chuoni kwa kuanza masomo Jumatatu 01 Juni 2020.
Dr. Avemarie Semakafu ameonyesha kuridhishwa na hatua za maandalizi na kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Chuo hicho, huku akiwataka elimu zaidi kuendelea kutolewa kujikinga na ugonjwa na hasa kwa wafanyakazi na wahadhiri wa chuo hicho.