Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amemshukuru kwa ushirikiano wake aliokuwa akimpa, aliyekuwa Naibu Waziri wake wa Afya, Dkt Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake ulitenguliwa jana na Rais Magufuli.
Hayo ameyabainisha leo Mei 17, 2020, kupitia ukurasa wake wa Twitter, na kumkaribisha kwa moyo wa dhati, Naibu Waziri wa Afya mpya Dkt Godwin Mollel, ambaye ameteuliwa siku ya jana.
"Asante Mh Faustine Ndugulile kwa utumishi wako na ushirikiano mkubwa ulionipatia katika kusimamia Sekta ya Afya nchini, kila la heri katika kuwatumikia wana Kigamboni, hongera Dkt Godwin Mollel karibu Wizara ya Afya, naahidi kukupa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao" ameandika Waziri Ummy.
Mapema leo asubuhi kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dr Faustine Ndugalile amemshukuru Rais Magufuli kwa Kumwamini kwa kipindi chote alichodumu kama Naibu Waziri Wizara ya Afya.
"Nimepokea uamuzi wa Mhe Rais kwa unyenyekevu mkubwa. Ninamshukuru sana JPM kwa kunipa fursa ya kuhudumu katika Serikali yake. Nawashukuru sana @umwalimu na watendaji wote kwa ushirikiano walionipatia.
Mafanikio ya sekta ni makubwa sana. Namtakia kila la kheri NW ajaye Dkt Mollel. "- Ameandika Ndugalile