Wizara ya Afya ya Rwanda imetangaza kifo cha kwanza kilichosababishwa na ugonjwa wa COVID-19 (corona) katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Katika taarifa ya leo Jumapili, wizara hiyo imesema aliyeaga dunia ni dereva wa lori mwenye umri wa miaka 65 na ambaye alikuwa amerejea nchini humo hivi karibuni kutoka nchi jirani ambako alikuwa anaishi.
Taarifa hiyo imesema mtu huyo ameaga dunia akipokea matibabu katika moja ya vituo maalumu vya kutibu ugonjwa wa COVID-19 nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Rwanda, watu 359 wameambukizwa virusi vya corona nchini Rwanda kufikia jana Jumamosi ya Mei 30. Aidha idadi ya wagonjwa wa corona waliopata ahueni nchini humo imeongezeka na kufikia watu 250.