Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATAHADHARISHA ‘TEGESHA’ NYAMONGO


Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Serikali imewatahadharisha wananchi wa kijiji cha Komarera kata ya Nayamongo Tarime Vijijini mkoani Mara kuacha tabia ya kufanya maendelezo maarufu kama Tegesha katika eneo linalotaka kuchukuliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa shughuli za uchimbaji madini.


Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara na Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha wakati wa kutangazwa notisi ya kusitisha kufanyika maendelezo kwenye vijiji vinavyozunguka Mgodi wa North Mara vya Kemorera na Kewanja vilivyopo wilayani Tarime na Mkuu wa wilaya Mtemi Msafiri.

Evelyne alisema, wakati mchakato wa kutwaa eneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini ukifanyika tayari baadhi ya wananchi wasio waaminifu katika maeneo ya Nyamongo wameanza kufanya maendelezo kwa kasi (Tegesha) kwa kupanda migomba na Mialovela lengo likiwa kujipatia fedha wakati wa zoezi la uthamini.

‘’Wananchi mmekosa subira kabisa mmeanza kupanda mialovera, migomba, miembe  na katani ili mjipatie fedha huko ni kutegesha na serikali haiko tayari kuwalipa watu wa aina hiyo, mimi kama mshauri wa uthamini nasema ni kosa kufanya hivyo’’ alisema Evelyne

Amewataka wananchi wa wameneo hayo hasa wanawake kutodanganywa kwa kushiriki kupanda vitu kwa kutegesha kwa kuwa havitahesabiwa na badala yake wote waliofanya hivyo waondoe walivyoapanda ili kuepuka hasara ya kutolipwa.

Akitangaza uamuzi wa kusitisha maendeleo kwenye eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Injinia Mtemi Msafiri alisema kuanzia siku ya kutangazwa notisi ya usitishaji hairuhusiwi mtu yoyote kufanya maendelezo na wananchi ambao vijiji vyao vinapitiwa na zoezi hilo wanatakiwa kusubiri zoezi la uthamini na atakayeenda kinyume atahesabika kama ametegesha

Alisema, Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara sasa unamilikiwa kwa ubia wa Kampuni ya Barick na Serikali kupitia Twiga Corporation Ltd na kusisitiza udanganyifu utakaofanyika utasababisha wananchi kutolipwa kwa wakati kama ilivyotokea kwenye zoezi la awali lililolazimu kufanyika uhakiki katika maeneo yaliyothaminiwa.

Kwa mujibu wa Mrakibu wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara Sadala Hamis eneo linalotakiwa kuchukuliwa kwa shughuli za uchimbaji madini kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo lina ukubwa wa takriban hekta 404 na wakazi wasioopungua mia tatu.

Hivi karibuni wakati wa kutoa fidia ya shilingi bilioni 33 kwa wakazi 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo la Nyamongo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazo Dkt Angeline Mabula alieleza kuwa zoezi la utoaji fidia lilichukua muda mrefu kwa sababu wananchi hawakuwa wakitoa taarifa sahihi na baadhi kutegesha na kuwaasa kutoa ushirikiano na kuwa wakweli katika masuala yanahusu ulipaji fidia sambamba na  kuwataka kutowekeza maeneo ambayo mgodi unataka kuyachukua.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com