Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Serikali Yataka Mikopo Ya Tadb Kuwa Chachu Kwa Wavuvi Kuanzisha Viwanda Vidogo.

Na. Edward Kondela
Serikali imesema inataka kuona uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi kupitia mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuyaongezea thamani mazao yanayotokana na sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezungumza hayo (30.05.2020) katika Kijiji cha Kanyala kilichopo Halmashauri ya Buchosa iliyopo Wilaya Sengerema Mkoani Mwanza, wakati wa kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 uliotolewa na TADB kwa Chama cha Ushirika cha Zilagula ambacho pia kimepata mkopo wa Shilingi Milioni Tano kutoka katika mfuko wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Mhe. Ulega amesema licha ya vyama vingine vya Kasalazi na Soswa ambavyo kila kimoja kimepata pia mkopo wa halmashauri wa Shilingi Milioni Tano, ili wafugaji na wavuvi waweze kunufaika na mikopo kupitia ushirika wao, wizara itakuwa msimamizi kwa vyama vitakavyokidhi sifa za kupata mikopo kutoka TADB.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaenda kuwa msimamizi namba moja wa vyama vya ushirika tena kwa barua hivyo niwatakeni uongozi wa mkoa, halmashauri na ushirika wekeni taarifa zenu vizuri. Tunataka viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi vikiwemo vya kukausha dagaa, minofu ya samaki na kutengeneza kayabo nzuri ili mpeleke bidhaa hizo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.”  Amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amevitaka vyama hivyo vitatu vilivyopata mikopo waitunze mikopo hiyo kwa kuifanyia kazi na hatimaye kuirejesha, kikiwemo Chama cha Zilagula kilichopata mkopo kutoka TADB, kwa kuwa fedha zilizotolewa na benki hiyo zinamilikiwa na watanzania kwa asilimia mia moja  ili watanzania wengine pia waweze kunuifaika na mikopo hiyo na kutoa rai kwa wavuvi kuendelea kujiunga katika vyama vya ushirika wakati akikabidhi hati ya kuandikishwa kwa vyama vya Sangara-Nyakaliro na Gembare vilivyopo Halmashauri ya Buchosa.

Amewataka pia watendaji wa serikali kutoa elimu kwa vyama vya ushirika namna ya kuitumia vyema mikopo wanayopata ili waweze kuirejesha kwa wakati pamoja na kuwaongoza ili waweze kupata mikopo mikubwa zaidi kwa kuwa utoaji mikopo kwa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kutaka kuona wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo hapa nchini.

“Watendaji wakati mwingine vyama vya ushirika havikosei kufikia hatua mbaya ya kukosa mikopo ni muhimu elimu itolewe na watendaji kwa wafugaji na wavuvi msiwaache hawa watu wa ushirika waliopatiwa mikopo kwa kuwapatia elimu na kuwaongoza hatua kwa hatua ili waweze kulipa marejesho ya mikopo waliyopatiwa.” Amefafanua Mhe. Ulega

Vilevile, Naibu Waziri Ulega amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kujiepusha na ubadhilifu wa fedha za mikopo hiyo kutoka TADB, huku akitoa rai kwa wavuvi kuwa na uchumi endelevu na hatimaye kuwa walinzi wa rasilimali za uvuvi kupitia vyama vyao vya ushirika kwa kuwa azma ya serikali ni kuona Tanzania inaongoza kwa kusafirisha minofu ya samaki kwenda nje ya nchi na mchango wa samaki katika pato la taifa unaongezeka kutoka Asilimia 1.7 hadi Mbili ya sasa na kufikia Asilimia Tano na kuendelea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka mikakati mizuri na benki hiyo iliyowezesha kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanakuwa na sifa za kupatiwa mikopo ili kujiendeleza katika sekta hizo.

“Tuliomba kwanza vyama hivi vikae katika ushirika kwa sababu tuliamini ule umoja wao utatupatia njia kuhakiksha mikopo inalipwa kwa kuwaweka katika mfumo ulio rahisi, wizara pia iliweka mazingira ya kubadilisha mitumbwi kuwa na namba na kufahamika ili benki iweze kuwa na taarifa sahihi ya mitumbwi ya wahusika wanaopatiwa mikopo pamoja na kuweka mazingira ya wavuvi kuwa na mifumo rasmi ya kuweka na kutoa pesa ili benki iweze kujua historia na kutoa mikopo kulingana na historia ya waombaji.” Amebainisha Bw. Justine

Bw. Justine ameongeza kuwa TADB inatoa mikopo hiyo na nia yao ni kuona wafugaji na wavuvi wengine wengi wananufaika na mikopo hiyo na kuwataka kufanya biashara zao kwa kuweka kumbukumbu zao vizuri ili wanufaika waweze kufikia hatua ya kuwa na viwanda vidogo vidogo.

Aidha, amesisitiza kwa vyama vya ushirika vilivyopata mkopo kutoka TADB kuhakikisha vinalipa mikopo hiyo kwa wakati ili watanzania wengine wenye uhitaji wa kupata mikopo hiyo waweze kupata na kukuza biashara zao.

Kuhusu Dawati La Sekta Binafsi lililo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambalo limekuwa likifanya kazi kubwa katika kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanaunganishwa na taasisi mbalimbali za kifedha, Mratibu wa dawati hilo Bw. Steven Michael amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha matokeo chanya yanaonekana likiwemo tukio la Chama cha Ushirika cha Zilagula kupatiwa mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kutoka TADB.

Bw. Michael amesema wamefanya kazi kubwa kuhakikisha vyama vya ushirika wanaviunganisha na taasisi za kifedha pamoja na halmashauri mbalimbali nchini na kufuatilia mara kwa mara kwa kuwa wao wanafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wadau wa mifugo na uvuvi na taasisi hizo kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Zilagula Bw. Joram Yuda amesema wanaishukuru serikali kwa kuwa wavuvi wameanza kuaminika na taasisi za kifedha kwa kuwapatiwa mikopo ili kujiendeleza katika sekta hiyo, huku Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Gembare Bw. Hassan Muhenga ameishukuru pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TADB kwa kuhakikisha wanasimamia maono ya Rais Dkt. John Magufuli ya wavuvi kupatiwa mikopo.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com