Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkoa wa Simiyu umezindua mpango mkakati wa kuwawezesha wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kusoma katika kipindi hiki cha likizo ya dharula ya tahadhari ya ugonjwa wa homa ya mapafu ( COVID 19) inayosababishwa na Virusi vya Corona.
Akizindua mkakati huo, Mei 04, 2020 katika Shule ya Sekondari Simiyu Mjini Bariadi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa mkakati huo utawasaidia wanafunzi kupata masomo wakiwa nyumbani kutoka kwa walimu wao huku ukiwa na malengo makuu manne yatakayoifanya Simiyu iendelee kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
" Malengo makuu ya mkakati huu ni kumwezesha mwanafunzi kuendelea kujifunza,walimu kuwa na mawasiliano ya kitaaluma na wanafunzi wao, wazazi kufanya ufuatiliaji wa taaluma kwa watoto wao pamoja na watoto(wanafunzi) kutulia nyumbani wakijisomea kipindi hiki cha likizo ambayo wako nyumbani; tahadhari zote za maambukizi ya Virusi vya Corona zitazingatiwa, "alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewataka wazazi na walezi kuwahimiza wanafunzi kutulia nyumba kujisomea na kufuatilia vipindi vya masomo mbalimbali vinavyorushwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini, huku akisisitiza maelekezo yote yanayotolewa na wataalam wa afya na viongozi juu ya tahadhari ya maambukizi ya Virusi vya Corona yazingatiwe wakati wa kujisomea.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl Ernest Hinju amesema Mkoa utaendelea kufanya mawasiliano na wazazi ili siku tatu baada ya shule kufunguliwa wanafunzi wapewe mitihani ili kuwapima.
Katika hatua nyingine mbunge wa jimbo la Bariadi, Mhe. Andrew Chenge ametoa msaada wa kompyuta tano na printa kwa Shule ya sekondari Simiyu kutoka mamlaka ya mawasiliano kwa wote ambazo zimekabidhiwa na Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa, Christina Chenge (mke wa mbunge huyo) kwa niaba ya mbunge.
Akikabidhi kompyuta hizo, Mama Christina Chenge amesema mbunge ametoa msaada huo na ametoa wito kuwa kompyuta hizo zitumike kwa kazi na malengo yaliyokusudiwa ili mkoa wa Simiyu uendelee kufanya vizuri katika sekta ya elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemshukuru Mhe. Chenge kwa msaada huo na misaada mingine ambayo amekuwa akiitoa kwa shule ya Sekondari Simiyu na shule nyingine ikiwemo saruji na mabati kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na mabweni na kusisitiza msaada huo kutumika kama ulivyokusudiwa.
Akiongea mara baada ya makabidhiano ya msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa hategemei kuona shule hiyo (Simiyu sekondari) iliyokabidhiwa vifaa hivyo kupata wanafunzi wenye daraja sifuri kwani tayari wana walimu na vifaa vya kutosha sambamba na madarasa ya kutosha.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Simiyu, Paul Susu amemshukuru Mhe. Chenge kwa kutambua uhitaji walionao kwani utawasaidia katika kutekeleza shughuli zao za ufundishaji huku akiongeza kuwa pamoja na kuwa shule ya Simiyu ndio imekabidhiwa shule nyingine zitanufaika pia kwa kuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano na shule nyingine.
Nao baadhi ya walimu wa shule hiyo akiwemo Dorine Bella na John Mogela wamesema kuwa ujio wa kompyuta hizo utakuwa chachu ya kurahisisha ufundishaji na kutekeleza mkakati wa mkoa wa wanafunzi kusoma katika kipindi hiki cha ugonjwa wa homa ya mapafu na baada ya ugonjwa huo.
MWISHO.
Social Plugin