Spika Job Ndugai jana alisoma barua ya Katibu wa Chadema, John Mnyika, iliyotaka bunge kutomtambua Cecili Mwambe kama Mbunge na kumlipa stahiki zake.
“Barua yenyewe ni fupi ngoja niwasomee, anasema Ceceli Mwambe, alikuwa mbunge wa jimbo la Ndanda aliyedhaminiwa na Chadema na Februari mwaka huu alitangaza kupitia vyombo vya habari amehama chama hicho,”alisema na kuongeza:
“Kwa mujibu wa ibara ya 7(f) ya Katiba amekoma kuwa mbunge na ameacha kiti chake katika bunge, kwahiyo bunge lisiendelee kumpatia stahiki zozote.”
Spika alisema anamshangaa Mnyika kwa kuwa maneno anayosema alipaswa aambatanishe na barua ya Mwambe inayothibitisha anayosema Mnyika na hajafanya hivyo.
“Pili sina barua ya Mwambe kusema kaacha ubunge kwa hiyari yake mwenyewe, na kama ni chama hiki kimechukua hatua sina viambatanisho vinavyoonyesha vikao halali vilivyofanya maamuzi haya, kwahiyo hii barua haina maana, haina mantiki,”alisema.
“Nawaambia wabunge wote ikiwamo wa Chadema mnaotishwatishwa huko kuwa mnaye Spika imara atawalinda mwanzo mwisho, habari ya ukandamizaji na ubabaishaji hauna nafasi, fanyeni kazi zenu kwa kujiamini, mmeaminiwa na wananchi,”amesisitiza
Social Plugin