Na John Walter-Manyara
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara (TAKUKURU) ,imefanikiwa kumrudishia Nyumba, mama mjane Antusa Duncan Kaaya,ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wilani Kiteto,akiitumia kujiingizia fedha kwa kuipangisha.
Imeelezwa kuwa Nyumba hiyo aliachiwa mjane huyo na mume wake aliefariki miaka minne iliopita, lakini muda wote amekuwa akiteseka huku mtumishi huyo wa serikali Katika idara ya Maendeleo ya jamii akiendelea kunufaika na mali za hizo.
Mama huyo anasema kwa kipindi chote hicho ameshindwa kuwalipia watoto ada kwa sababu nyumba hiyo ndio ilikuwa tegemeo la familia katika kupata kipato.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu amesema kumekuwepo na vitendo vichafu vya watumishi kuwadhulumu haki zao wananchi wanyonge na wao kama mamlaka wamebaini kuwepo kwa vitendo hivyo na kwamba wataenda sambamba na watu wa aina hiyo.
Amesema afisa huyo alipaswa kusaidia jamii kupata haki yake lakini badala yake amekuwa sehemu ya kuikandamiza jamii hivyo akiwa kama Kamanda wa TAKUKURU Manyara atahakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua zaidi.
Akikabidhi mali hiyo kwa mjane huyo,mkuu wa wilaya ya Kiteto Tumaini Magesa amesikitishwa na kitendo hicho cha mtumishi huyo kudhulumu mali zake na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi yake.
Wananchi wameipongeza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara (TAKUKURU) kwa hatua hiyo ya kumrudhishia haki yake mama huyo mjane.
Social Plugin