Ndugu Wananchi
Kila tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaliamuliwa mwaka 1972 katika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu masuala ya Mazingira, uliofanyika katika Mji wa Stockholm nchini Sweden. Mkutano huo uliazimia kwamba tarehe 5 Juni, kila mwaka iwe ni siku ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.
Ndugu Wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali na umuhimu wa hifadhi ya mazingira katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za hifadhi mazingira na mbinu/njia mbalimbali za kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Upotevu wa bioanuai, uharibifu wa tabaka la ozone, na shughuli nyingine mbalimbali zinazochangia uharibifu wa mazingira
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu Taifa letu linakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi yasiyoendelevu ya rasilimali za kimazingira. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na uharibifu wa ardhi, ufyekaji na uharibifu wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini na upotevu wa bioanuai. Changamoto hizi kwa ujumla zinasababisha athari kubwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana na changamoto hizi serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekua ikichukua hatua mbalimbali ili kupambana na hali hii. Mojawapo ya njia za kupambana na changamoto hii ni kutumia Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani ili pamoja na mambo mengine kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.
Ni kwa muktadha huu, Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani kitaifa yalipangwa kufanyika mkoani Lindi mwaka huu. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Kauli mbiu hii inaakisi hali halisi ya nchi yetu kuathirika na mabadiliko ya tabianchi. Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ukame mkali na wa mara kwa mara pamoja na mafuriko ambayo yamekua yakiikumba nchi yetu na kusababisha hasara kubwa ya miundombinu, makazi ya watu na hata vifo katika baadhi ya sehemu za nchi yetu.
Mfano wa hivi karibuni mafuriko yaliyoukumba mkoa wa Lindi na kusababisha hasara kubwa takriban vijiji 16 viliathiriwa na mafuriko hayo pamoja na watu 19 kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo.
Aidha, takriban watu 15,000 wamekosa makazi pamoja na uhaba wa chakula na kuathiriwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Kaulimbiu hii inahimiza jamii kutumia mbinu mbalimbali za asili na za teknolojia rafiki za kuhifadhi mazingira ikiwemo kilimo cha matone, nishati mbadala, ufugaji wa mifugo chotara na upandaji wa miti ya asili kwenye vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu, Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona. Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watu.
Uwepo wa janga hili umesababisha kusitishwa kwa shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu. Aidha, kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kwamba mwaka huu hapatakuwepo na mikusanyiko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa yaliyopangwa kufanyika mkoani Lindi.
Kwa muktadha huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya wiki ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Aidha, kila Mkoa utafanya shughuli za maadhimisho hayo kwa kutumia vyombo vya habari vilivyopo kwenye maeneo yao pamoja na mitandao ya kijamii kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na:
mashindano ya kuandika insha zinazohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hotuba za viongozi, jumbe mbalimbali zitakazotumwa kwenye mitandao ya simu pamoja mikutano ya kitaalamu kuhusu mabadiliko ya Tabianchi ambayo itafanywa kwa njia ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Ndugu Wananchi,
Ni vyema ikafahamika kwamba hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali pekee yake bali ni jukumu letu sote katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya. Nitoe wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia tusaidiane katika kuhifadhi mazingira.
Watendaji wote katika ngazi zote hatuna budi kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini.
Ningependa kusisitiza kuwa tushirikiane katika kufanya jitihada mbalimbali ili kupambana na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kila mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira yetu na jamii kwa ujumla. Kwa muktadha huu, shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira hapa nchini mwaka huu pamoja na mambo mengine, zitalenga kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuelimishana jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Ndugu Wananchi,
Napenda kuwapongeza, wadau mbalimbali wa Mazingira ambao ni UNDP, UNEP, WWF, GIZ, Forum CC, Vodacom Foundation, USAID na nchi wahisani pamoja na vyombo vya habari kwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha na kuelimisha jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa kuhifadhi Mazingira.
Mwisho, natoa wito kwa Mikoa yote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwenye mikoa yenu kuhamasishana na kuelimishana masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira sambamba na kuepuka mikusanyiko ya watu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Mussa Azzan Zungu (Mb.),
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS
(MUUNGANO NA MAZINGIRA)
18/05/2020
Social Plugin