Tanzania imetangaza rasmi kufungua anga lake ambalo lilikuwa limefungwa kutokana na ugonjwa wa covid 19 ambapo kwa sasa ndege zote zikiwemo za watalii na kibiashara zipo huru kuingia Tanzania.
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano Mhe Isack Kamwelwe akizungumza jijini Dodoma pia ameliagiza Shirika la ndege Tanzania (ATCL) kujipanga ili kurejesha Huduma za usafari kwa nchi ambazo zimefungua Anga zao.
“Baada ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa huo hapa Tanzania kama ilivyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jana mai 17, 2020, imebainika kuwa udhibiti wa ugonjwa huo umeendelea kuimarika
” Kwamba wagonjwa wamekuwa wakipungua katika vituo mbalimbali vya afya nchini hivyo Serikali inatangaza kufungua anga lake rasmi kuanzia leo tarehe 18, mei, 2020″ amesema Kamwelwe.
Amesema kuanzia sasa ndege zote za kibiashara, misaada, kidiplomasia , dharura na ndege maalumu zinaruhusiwa kuruka, kutua, na kupita juu ya anga la Tanzania kama ilivyokuwa awali.
Aidha Mhandisi Kamwelwe amebainisha kuwa taratibu za kiafya zilizowekwa na shirika la afya ulimwenguni (WHO) pamoja na Wizara ya Afya zitazingatiwa wakati wote.
Amesema watahakikisha abiria wote wanaoingia na kutoka watapimwa joto na endapo watahisiwa kuwa na viashiria vya virusi vya Corona watawekwa sehemu maalumu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Pia ameagiza mamlaka ya usafiri wa anga (TCAA) kuliarifu Shirika la anga la kimataifa kuhusu maamuzi haya na kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa bila vikwazo vyovyote.
Social Plugin