Mtoto mwenye umri wa miaka minane (jina tunalo) ambaye alizaliwa na tatizo la moyo aliloishi nalo kwa miaka yote hiyo, ametibiwa kwa mafanikio katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mtoto huyo aliyezaliwa pacha (wawili) alikuwa anakabiliwa na matatizo ya aina mbili ya moyo ikiwamo lile la tundu dogo kwenye vyumba viwili vidogo vya moyo, pamoja na mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa kuziba na kusababisha damu kushindwa kusafishwa vizuri.
Akizungumza kuhusu matibabu ya mtoto wake mama mzazi wa mtoto huyo Stamil Abdallah ambaye ni mkazi wa Mkoani Ruvuma alisema kwa kipindi cha miaka nane mwanae alikuwa akiteseka na maradhi ya moyo hivyo kupelekea ukuaji wake kuwa wa tofauti ukilinganisha na ule wa pacha wake.
“Nilikata tamaa kama mtoto huyu atakuwa na afya njema kwani kwa hali aliyokua nayo alikuwa anazimia mara kwa mara, moyo kwenda mbio, anachoka na kubadilika rangi katika vidole vya mikono yake na ulimi hali hii ilinipa wasiwasi, lakini sasa namshukuru Mungu mwanangu anaendelea vizuri”, alisema Stamil.
“Nawashukuru sana wadau mbalimbali waliojitokeza kuokoa maisha ya mwanangu kwani mimi ninatokea katika familia yenye uwezo mdogo kiuchumi. Baada ya mwanangu kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Peramiho na kugundulika kuwa na matatizo ya moyo nilikata tamaa kwakuwa sikujuwa ni wapi ningepata fedha za matibabu”,.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema mtoto huyo alizaliwa na matatizo mawili, la kwanza ana tundu kati ya upande wa vyumba vidogo vya kushoto na kulia na tatizo la pili ni mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa ulikuwa umeziba na kusababisha damu kushindwa kusafishwa vizuri.
Prof. Janabi alisema kutokana na tatizo hilo damu ilikuwa haiwezi kwenda kwenye mapafu ili damu chafu iweze kusafishwa kuchukua damu safi iweze kurudi kwenye moyo, ndiyo maana baadhi ya viungo vya mwili wake ikiwemo mikono, kucha, ulimi na miguu vilikuwa na rangi ya bluu.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji amebadilika kabisa amekuwa wa pinki, ulimi na kucha zimerudi katika hali ya kawaida, tumempa tena nafasi ya kufurahia maisha, atandelea na masomo yake na kuweza kucheza na wenzake kama wanavyofanya watoto wengine,”.
Naye Mkuu wa Idara ya watoto ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Sulende Kubhoja alisema watoto wenye matatizo kama hayo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha damu vizuri wako wengi ambao wanapokelewa na kutibiwa katika Taasisi hiyo.
Dkt. Kubhoja alisema wamefanikiwa kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua na kuzibua mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa uliokuwa umeziba na kusababisha damu kushindwa kusafishwa vizuri. Baada ya kufanyia upasuaji kiwango cha oxygen mwilini kimepanda kutoka asilimia 60 hadi kufikia asilimia 100.
“Ninawashauri wazazi kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kuwapeleka watoto kliniki baada ya kujifungua hii itawasaidia kugundulika mapema kama wanamatatizo ya moyo na kuweza kupata matibabu kwa wakati”, alisema Dkt. Kubhoja.
Upasuaji wa bila kufungua kifua huwa unafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika mshipa wa damu ulioko kwenye paja.
Social Plugin