Na Faustine Gimu
WAZIRI wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano mhandisi ISAACK KAMWELWE amesema ndege ya kwanza iliyobeba watalii kutoka Ugiriki imetua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA)baada ya kufungua anga ya Tanzania.
Hatua hiyo imefuatia baada ya serikali kuruhusu ndege zote za kibiashara,misaada,kidiplomasia ,ndege za dharura na ndege maalum kuruka,kutua na kupita juu ya anga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mei 21,2020 ofisini kwake jijini Dodoma kuhusu mikakati iliyochukuliwa ili kuimarisha usalama katika usafiri wa majini nchini ,Mhandisi KAMWELWE amesema hatua hiyo ni mwanzo wa kurejea kwa usafiri wa anga kwa ndege za Kimataifa.
“Ndege iliyotua ilikuwa na watalii wanne na crew ya watu watatu na wametua tayari, wamepokelewa na wamekwenda kuangalia wanyama,” alisema.
Aidha, alisema anaratiba ya ndege zitakazofanya safari zake kuja Tanzania na booking zimejaa, huku akisisitiza ifikapo Mei, 28, mwaka huu ndege nyingi zaidi zitatua ikiwamo zilizobeba watalii.
“Yapo mashirika ya ndege yalishajiandaa kama Emirate, Ethiopia, KLM na kwa upande wa zitakazofanya safari za mizigo tulianza na Rwanda Airline kuanza kubeba minofu ya samaki, leo (jana) tumeongeza ndege nyingine Ethiopia Airline ambayo itabeba tani 19 za minofu ya samaki,” alisema.
Aidha, waziri huyo alisema Jumapili (Mei 24), ndege ya Ethiopia itarudi tena jijini Mwanza na kubeba tani 40 ya minofu ya samaki.
“Tunaendeleza mazungumzo uwanja wa Mwanza umefunguka na kwa kuwa ni uwanja wa kimataifa, ndege zitaruka kimataifa kwa ajili ya kubeba mizigo na tunaendelea kuongea na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na nyama ianze kusafirishwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Kamwelwe alisema Shirika la Ndege (ATCL) linakamilisha taratibu za kuanza kubeba na kupeleka mizigo Ulaya kwa ajili ya biashara.
Ikiwa sasa ni miaka 24 tangu kutokea kwa ajali ya MV Bukoba iliyosababisha watu takribani 800 kupoteza maisha mhandisi KAMWELWE amesema serikali imeendelea kujidhatiti ili kuimarisha usalama wa usafiri wa majini ikiwemo kuboreshwa kwa Sheria na Mamlaka ya Udhibiti ya Usafiri Majini.
Ametaja mikakati mingine kuwa ni uboreshwaji wa mafunzo na utoaji wa vyeti vya mabaharia na kuendelea kuimarisha ushirikiano na Shirika la Bahari Duniani katika kutekeleza itifaki za kimataifa zinazosimamia usafiri wa Bahari Duniani.
Amesema kwa kutekeleza mambo hayo matano ni imani yake kuwa sasa usalama wa usafiri kwa njia ya maji ni salama na utaendelea kuwa salama chini ya usimamizi wa wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.
Social Plugin