WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAOMBA KUIDHINISHIWA ZAIDI YA TSH. BILIONI 81.4

Na.Faustine Gimu,Dodoma

Serikali imeendelea  kuhamasisha wananchi kununua bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya ndani  ili kujenga uchumi wa nchi ambapo  Katika mwaka 2019/2020, jumla miradi mipya 303 imesajiliwa.

Hayo yamesemwa jana  Mei,5,2020  jijini Dodoma na   Waziri wa  Viwanda na Biashara Mhe. Innocent   Bashungwa  Wakati akiwasilisha Bungeni  Hotuba ya Makadirio Ya Mapato na Matumizi Ya Fedha Kwa Mwaka 2020/2021   ambapo amesema Serikali imeendelea kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha vinapata malighafi ya kutosha kwa kutoza ushuru mkubwa, kuweka katazo kwa baadhi ya malighafi kwenda nje ya nchi na kutoa vibali maalum kwa baadhi ya bidhaa.

Katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unayosababishwa na virusi vya Corona  [Covid-19 ], Mwezi Machi 2020, Wizara ilikutana na wazalishaji wa malighafi ya kutengeneza vitakasa mikono na wazalishaji wa bidhaa hizo ambapo inaendelea na  ufanyaji tathmini ya mahitaji ya vitakasa mikono nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Mkemia Mkuu wa Serikali, Wazalishaji wa Vitakasa mikono , TMDA na TPMA.

Aidha,  Waziri Bashungwa amesema kupatikana kwa takwimu halisi  kutasaidia Serikali kufanya maamuzi ya haraka hususan ya kuagiza Ethanol ambayo ni malighafi muhimu katika kutengenezea vitakasa mikono  huku akitoa onyo kwa wafanyabiashara wanaotumia mazingira ya ugonjwa huo kama fursa ya kujinufaisha badala ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na Janga hili .

 Akiwasilisha Taarifa Ya Kamati Ya Kudumu Ya Bunge Ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Utekelezaji Wa Majukumu Ya Wizara Ya Viwanda na Biashara, Fungu 44-Viwanda Na Fungu 60-Biashara Kwa Mwaka 2019/2020 na Maoni Ya Kamati Kuhusu Makadirio Ya Mapato na Matumizi Fungu 44 Na 60 Ya Mwaka Wa Fedha 2020/2021 Makamu Mwenyekiti Kamati Ya Bunge Ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kanal Mstaafu,Masoud Ally Khamis ameishauri serikali kufuatilia kwa ukaribu mapato ya  makusanyo ya maegesho ya Magari na Makontena katika eneo la  Kurasini ili kubaini  kama fedha zilizokuwa zinakusanywa zilikuwa zinafika katika mfuko mkuu wa serikali.

Wakichangia hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara  ,Mbunge  wa Geita Vijijini Joseph Msukuma ametaka serikali kuchukua maamuzi ya kuwafungulia wawekezaji,ambapo mbunge wa viti Maalum Zainab Mndolwa ameishauri serikali kuona namna ya kuwapunguzia kodi  wafanyabiashara kutokana  janga la Corona huku Mbunge wa Bagamoyo akishauri wananchi kurejeshewa kurejeshewa maeneo ambayo hayakuendelezwa .

Kwa mwaka 2020/2021, Wizara ya Viwanda na Biashara  imeomba kuidhinishiwa  jumla ya Shilingi  Bilioni  themanini na moja ,milioni  mia tatu sitini na sita  ,laki tisa na elfu mbili [ 81,366,902,000] ambapo  Kati ya fedha hizo, zaidi ya  Shilingi  Bilioni 51.7 ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi  bilioni 29.7 ni za Matumizi ya Maendeleo.

Aidha,Katika mwaka 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya Shilingi  Bilioni 15 kutokana na uuzaji wa nyaraka za zabuni .

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post