Na Jackline Lolah - Malunde 1 blog Morogoro
Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Willbroad Mutafungwa amewataka wananchi wanaojihusisha na kilimo cha bangi kuacha mara moja huku akitoa siku mbili kwa viongozi wa vijiji vitano mkoani Morogoro kujisalimisha polisi baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi hilo kubaini hekari 100 za mashamba ya bangi.
Kamanda Mtafungwa alitoa agizo hilo jana wakati wa operesheni maalum ya kusaka watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu vya kuzalisha na kuuza bangi kinyume na sheria.
Alisema mashamba hayo zaidi ya hekari 100 yamebainika umbali wa kilomita 30 kutoka eneo la makazi ya watu katika kijiji cha Misengele, Tarafa ya Doma.
"Ndani ya wiki moja kuanzia tarehe 1juni hadi tarehe 8 mwezi Juni mwaka huu tumefanya oparesheni maalumu ya kudhibiti dawa za kulevya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12 wa makosa mbalimbali ya bangi ambapo vilivyopatikana ni viroba 5 na nusu, misokoto 160 ya bangi na puli moja na nusu, kete 10 za bangi na gari yenye namba za usajili T. 572 CFN aina ya Toyota Brevis rangi ya silva, pikipiki 2 aina ya houjue na ekari 100 ya mashamba ya bangi",amesema.
“Natoa siku mbili kwa viongozi hawa wa jijiji vya Bunduki, Misengere, Kododo, Vinile, na Yowe, kata ya Doma, wilayani Mvomero, vinavyozunguka bonde la Mto Mgeta kujisalimisha kituo cha polisi wenyewe ili watuambie walikuwa wapi miaka yote mambo haya yanafanyika katika maeneo yao pasipo kutoa taarifa yoyote,” alisema Mutafungwa.
Alisema eneo hilo lililopo karibu na mto Mgeta, lipo ndani ya hifadhi ya msitu asilia wa Misengele na kuzitaka mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa maeneo hayo kuweka uangalizi wa karibu kujua shughuli zinazoendelea.
“Eneo hili ni hifadhi hairuhusiwi mtu yeyote kufika ama kuendesha shughuli za kibinadamu, lakini katika operesheni kufuatilia taarifa za uchunguzi inabainika uwapo wa mashamba haya makubwa ilhali viongozi wa vijiji wapo na wamenyamaza,” alisema Kamanda Mtafungwa.
Kamanda Mtafungwa alisema katika operesheni hiyo inayoendelea watu 12 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Social Plugin