Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina akizungumza na wandishi wa habari na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Sehemu ya Wadau wa maziwa wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina wakati wa kujadili mambo mbalimbali ya sekta ya maziwa katika wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Patrobas Katambi,aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akizungumza na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote akizungumza na wadau wa bodi ya maziwa wakati wa ufungaji wa kilele cha siku wiki ya maziwa.
Mwenyekiti wa Baraza la wadau ni Bi.Catherine Dangat,akizungumza na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (wa pili kushoto) akinywa maziwa kuashiria kufunga wiki ya maziwa nchini sambamba na Viongozi wengine akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (wa tatu kutoka kushoto) na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote (katikati).
..............................................................................................
Na. Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imeitaka Bodi ya Maziwa na Wadau wote wa maziwa kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha ndani ya miaka miwili ijayo Tanzania inazalisha maziwa ya kutosha ili kusiwe na haja ya kuagiza maziwa nje Nchi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina leo jijini Dodoma wakati akihitimisha wiki ya Maziwa duniani ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye viwanda vya kusindika maziwa kuongeza uzalishaji zaidi.
Mhe. Mpina amesema kiwango cha kunywa maziwa kwa watanzania kinapaswa kuwa Tani 200 lakini hadi sasa kiwango kinachonyweka ni tani 54 hivyo kuwataka watanzania kuongeza unywaji wa maziwa kwani husaidia kuboresha kinga za mwili na kukuza ubongo.
Mhe. Mpina amesema kuwa ili kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongeza serikali imewaunganisha wawekezaji wa maziwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupatiwa mifugo sambamba pia na kutoa msamaha wa kodi kwenye sekta hiyo.
" Ndugu zangu ni muda sasa wa kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwani Maziwa ni mlo kamili hasa katika kuimarisha mifupa na kuweka ubongo sawa, na yana viini lishe vya kuimarisha pia kinga za mwili”, amesisitiza Mhe. Mpina.
Aidha Mhe. Mpina ameweka wazi kuwa Tanzania ni Nchi ya pili kwa kuwa na Ng'ombe wengi nyuma ya Ethiopia kuwa Tanzania ina Ng'ombe Milioni 33 lakini Ng'ombe wanaozalisha maziwa ni Milioni 1.9 na kiwango cha maziwa kinachozalishwa ni Bilioni tatu ambacho ni kidogo kulinga na mifugo tuliyinayo.
Mhe. Mpina amesema kwa sasa kuna programu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni kwa baadhi ya mikoa na kusisitiza sasa ni wakati wa kila mkoa kuweka mkakati wa kuhimiza unywaji wa maziwa kwenye kila shule ndani ya mikoa yao.
Pia Mhe. Mpina ametoa wito kwa wawekezaji nchini kutumia fursa ya kuwekeza kwenye usindikaji wa maziwa kwani viwanda vilivyopo kwa sasa vinazalisha asilimia 23 tu ya maziwa na vipo 99.
Mhe. Mpina amehitimisha kwa kuelekeza Halmashauri zote nchini kuzingatia bei elekezi ya chanjo ya mifugo na atakayekaidi hatua kali za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake
Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote amesema wiki ya Maziwa imekua ya manufaa sana kwani wiki hii waligawa Lita 1650 kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Mrote amesema kuwa ndani ya wiki hiyo ya maziwa walikutana wadau wote wa maziwa na kujadili mambo mbalimbali yatakayoweza kuivusha sekta hiyo ili kufikia hatua ya kuzalisha maziwa mengi na kukuza soko hilo hadi nje ya mipaka ya Nchi.
Social Plugin