Chama cha Wananchi - CUF kimesema ratiba yao ya kura za maoni na uteuzi wa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais imeanza tangu mwezi Mei ambapo inatarajiwa kuhitimishwa tarehe Julai 27, ambapo agombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho Bara na Zanzibar watatateuliwa.
Hayo yamesemwa jana tarehe 6 Juni 2020, na Juma Killghai, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, alipokuwa akitoa ratiba ya kuwapigia kura za maoni na uteuzi watia nia wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu 2020.
Alisema chama hicho kimejidhatiti kusimamisha wagombea wa nafasi zote nchi nzima na kuwataka wanachama wote wenye sifa kujitokeza kugombea.
“Tunatarajia kuweka wagombea nchi nzima katika ngazi za udiwani, uwakilishi na ubunge.
“Aidha, tunatarajia kusimamisha wagombea Urais wawili, mmoja akisimama kwa ajili ya Urais wa Zanzibar na mwingine akisimama kwa ajili ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Aidha Killghai alisema chama hicho kitashirikiana na chama chochote chenye dhamira ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani.
“Chama chetu kipo tayari kushirikiana na chama chochote chenye dhamira ya kweli ya kuiondoa CCM na kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi, isiwe kinaingia madarakani kinafanya yaleyale yaliyokuwa yakifanya na CCM,” alisema
Alisema, mchakato wa kugawana majimbo ama kata utafanyika kwa utaratibu watakaokubaliana baina yao na chama ambacho kitaafikiana nacho.
Social Plugin