Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF) limemsimamisha Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Abbas Juma Muhunzi kwa kukiuka maadili ya uongozi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwaUmma CUF, Mohamed Ngulangwa inaeleza kuwa, kwa kuzingatia Ibara za 83(1) (b) na 94(1) zinazolipa Baraza Kuu la uongozi la Taifa mamlaka na muongozo katika kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa viongozi wakuu.
Baada ya wajumbe kupokea tuhuma dhidi ya Muhunzi na kufanya mjadala wa kina, Baraza hilo lilitoa nafasi kwa mlalamikiwa kujitetea ambapo alikiri kufanya makosa yaliyoelekezwa kwake na akakiachia kikao kuamua dhidi yake.
Wajumbe katika kikao hicho waliamua kupiga kura za kumsimamisha uongozi ambapo wajumbe 42 walitaka Muhunzi asimamishwe huku wajumbe 7 wakipinga kumsimamisha na wajumbe 6 hawakuunga mkono wala kupinga kusimamishwa kwa Muhunzi.
Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, maamuzi ya kumsimamisha Muhunzi yanastahili kufikishwa kwenye mkutano mkuu kwa maamuzi ya mwisho ndani ya siku 90 kuanzia leo.