Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MBOGWE AWASHUKIA WATENDAJI WANAOKWAMISHA MAENDELEO YA WANANCHI

SERIKALI Wilayani Mbogwe Mkoani Geita imewataka watendaji wa halmashauri hiyo pamoja na viongozi wengine katika chama kutowakatisha tamaa wananchi wenye wanaojitolea nguvu zao katika zoezi la utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Martha Mkupasi aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na kamati ya shule ya msingi Kanegere iliyopo Kata ya Bukandwe wilayani Mbogwe alipoongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kujionea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyoo 18 katika shule ya msingi Kanegere iliyopo Kata ya Bukandwe. 

Katika shule hiyo Mkupasi alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Milioni 27. 9 huku akisisitiza kuwa serikali yake imepokea fedha kiasi cha shilingi Milioni 175 ambazo kwa sasa zinatekeleza mradi mkubwa wa vyoo 177 kwenye shule 7za msingi ikiwemo shule ya msingi Kanegele iliyotengewa Milioni 27.9 kwaajili ya ujenzi wa vyoo 18.

“Namshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kusikia kilio chetu na kutupa fedha za ruzuku kutoka serikali kuu, Milioni 175 siyo nawaagiza watendaji wa Halmashauri fedha hizo zitumike kama ilivyopangwa asitokee mjanja mmoja akakwamisha shughuli nzima naamini mradi huu utakwenda hadi miezi miwili,” alisema Mkupasi na kuongeza.

“Ndugu zangu wananchi vyoo vya kisasa vinajengwa katika shule zenu naamini suala la kujisaidia vichakani halitakuwepo tena, licha ya shule ya msingi Kanegere kuanza kuchimbwa mashimo kwaajili matundu ya vyoo, kwa sasa kuna hatua nzuri kutokana na ushirikiano mzuri na wananchi wanaojitolea nguvu zao,” alisema Martha mkupasi mkuu wa Wilaya ya Mbogwe.

Aliwahakikishia wananchi wake kuwa mradi wa vyoo vya kisasa katika wilaya hiyo utakuwa wa mfano hapa nchini huku akitamba kuwa halmashauri zingine pindi mradi huo utakapokamilika watatua kuja kujifunza na kutumia fursa hiyo kuwaomba wananchi waendelee kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuhamasika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Licha ya fedha za Ruzuku Milioni 175 kutoka serikali kuu pia katika mwaka wa fedha ujao serikali kupitia Halmashauri ya Mbogwe imetenga zaidi ya shilingi Milion 200 kwaajili ya ujenzi wa vyoo ili kukabiliana na upungufu",alisema.

Nae afisa elimu takwimu na vifaa wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Frolence Leodigard akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya kwa niaba ya afisa elimu msingi Wilaya Peter Buvuva alisema kuwa shule ya msingi Kanegere ni kati ya shule saba zinazonufaika na mradi huo na imetengewa kiasi cha shilingi Milioni 27.9 ili kutekeleza ujenzi wa vyoo vya kisasa.

“Kwa wilaya nzima upungufu wa matundu ya vyoo ni 3178, vilivyopo ni 815 na katika shule hii ya Kanegere ina jumla ya wanafunzi 1,147 wasichana ni 585 na wavulana wakiwa 562 kwa hiyoa matundu 16 ya vyoo yaliyopo shuleni hapo hayatoshelezi idadi hiyo, mahitaji ni matundu 51, yaliyopo ni 11,” alisema Leodigard.

Akizungumzia mradi huo afisa mtendaji wa Kata ya Bukandwe Muberwa Bakalemwa alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wananchi wa eneo hilo wamepokea mradi huo kwa shangwe kubwa huku akibainisha kuwa kutokana na wananchi kufuata mchanga umbali mrefu waliruhusiwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS wilaya ya Mbogwe kuzoa katika moja ya hifadhi baada ya kuwaandikia barua.

“Sisi kamati ya shule ya msingi Kanegere tulihamasisha wazazi na wananchi wengine kujitolea nguvu zao ambapo kupitia vitongoji vyao na kijiji kwaujumla wananchi waliguswa na hali ya uhaba wa vyoo na sasa wamejitolea kuchimba mashimo kwaajili ya matundu ya vyoo ikiwemo kusomba mchanga makarai matatu kila mwananchi pamoja na mawe ambayo kwa sasa yapo ya kutosha,” alisema Samweli Shitungulu mwenyekiti kamati ya shule.

Mkuu wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Martha Mkupasi aliyeongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kujionea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matundu vyoo 18 katika shule ya msingi kanegere iliyopo Kata ya Bukandwe.




 Wananchi wa Kata ya Bukandwe wakijitolea nguvu zao katika kushiriki ujenzi wa vyoo hivyo  ili kukabiliana na uhaba uliopo katika shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule saba inayonufaika na mradi wa Milioni 175 kutoka serikali kuu huku shule hiyo ikitengewa shilingi Milioni 27.9 kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo wa vyoo vya kisasa,  na vyoo vinavyoonekana ni vya zamani.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com