Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GARI YA TANAPA YAGONGA NA KUUA WATU WATATU BABATI

Na John Walter-Babati
Watu watatu  wamekufa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kata ya Mamire  wilayani Babati mkoani Manyara.

Akitoa taarifa leo June 16.2020, Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara Paul Kasabago amesema, ajali hiyo iliyotokea june 13 mwaka huu,  imehusisha gari  lenye namba za usajili SU.417 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya shirika hifadhi za Taifa (TANAPA),  iliyokuwa  katika doria maalum katika maeneo hayo yanayopakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire majira ya saa 2:45 usiku.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara Paul Kasabago akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, amesema gari hilo lililokuwa linaendeshwa na dereva ambaye bado majina yake hayajafahamika, iligonga pikipiki yenye namba za usajili MC 313 BKU aina ya Boxer iliyokuwa ikiendeshwa na Said Ally (35) mkazi wa Mamire akiwa amewapakia abiria wawili (mshkaki) kinyume na sheria za usalama barabarani.

Kasabago amesema kuwa dereva wa pikipiki hiyo na abiria wote wawili aliokuwa amewabeba walipoteza maisha papo hapo.

Aidha Kamanda Kasabago ametaja majina ya waliopoteza maisha ni Said Ally (35), Elimina Herman (22) na Renatha Salutali (17) wote wakazi wa kijiji cha Mamire.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Paul Kasabago, mtuhumiwa alitoroka mara baada ya kusababisha ajali hiyo  na kwamba  jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi  wanaendelea kumtafuta ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kamanda ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo kushindwa kuchukua tahadhari za usalama bara barani.

Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi wa kidaktari  na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com