Na Mwandishi Wetu
Katika kukuza sekta ya elimu ya juu nchini, Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd. (GGML) kupitia sera yake ya uwajibikaji kwa jamii imetoa kiasi cha Sh milioni 100 kusaidia ujenzi wa Kituo cha Chuo Kikuu Open University cha Mkoa wa Geita.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa jengo la utawala linalojumuisha chumba mikutano cha viongozi, maktaba, chumba cha maabara ya kompyuta na ofisi nyingine tano.
Pia kiasi hicho cha pesa kilichotolewa na GGML ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi na malipo ya mafundi ujenzi.
Akizungumzia mradi huo, Makamu Rais - Maendeleo Endelevu katika kampuni hiyo, Simon Shayo alisema uwezeshaji huu unatarajiwa kufaidisha wanafunzi 500 wanaotokea katika vituo vitatu vya Mkoa wa Geita ambavyo ni Chato, Nyang’wale na Geita mjini.
Alisema GGML kwa kushirikiana na wananchi imeamua kuunga mkono juhudi za serikali kufadhili mradi huo kwani mbali na kuongeza mazingira bora ya upatikanaji wa elimu pia utazalisha wahitimu bora wenye weledi ndani ya jamii wataokuwa na uwezo wa kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele kwa kupitia elimu waliyoipata.
Alisema Chuo cha Open University - Geita, kama vilivyo vyuo vingine kimekuwa kikifanya shughuli zake katika majengo ya kukodi ambayo hutumika kama madarasa na ofisi za utawala.
“Mradi huu unaifanya Geita kuwa mkoa wa (1, 2, 3) katika ukanda wa ziwa na wa (2, 10, 20) nchini Tanzania kunufaika na miundombinu inayomilikiwa wa Open University.
"Kwa ufadhili huu, tuna hakika kwamba chuo kikuu kitapunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ufanisi. Zaidi ya hayo itaunda uhusiano mzuri kati ya wanafunzi kutoka Geita na vyuo vingine 30 vya Open University Tanzania. Mradi huu moja kwa moja unasaidia Serikali kufikia lengo la 4 la maendeleo endelevu (SDGs), ambalo ni upatikanaji wa elimu bora ifikapo 2030 kama ilivyotarajiwa ”alisema Shayo.
Aidha, Mkurugenzi wa Open University Geita, Ally Abdu aliishukuru GGML kwa msaada huo ambao unaongeza mazingira mazuri ya kusoma na kukidhi idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu ambao wanaongezeka kila mwaka.
"Malengo ya Chuo kikuu huria ni kutoa elimu inayofaa na yenye ubora, elimu iliyo rahisi kupatikana na nafuu kwa njia ya mtandao. Elimu iliyojitosheleza kwa tafiti zenye kutoa suluhu ya matatizo ndani ya jamii kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.
“Kupitia msaada huu wa GGML, sasa tuna uhakika kwamba tutapunguza gharama zetu za uendeshaji na kuboresha ubora wa elimu katika tawi letu la Geita, " alisema Ally.
Hata hivyo, Shayo aliongeza kuwa kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017, Kampuni ya Dhahabu ya Geita kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii imeungana na serikali za mitaa za Geita kutekeleza miradi ya jamii yenye thamani ya Sh bilioni 18 katika Mkoa wa Geita.
“Kabla ya marekebisho GGML ilikuwa imewekeza kihistoria katika miradi endelevu ya kimkakati kwa jamii ikiwa ni pamoja na shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, mradi wa maji safi wa mji wa Geita na mradi wa Kilimanjaro Challenge unaolenga kutokomeza maambukizi ya VVU/UKIMWI nchini,” alisema.
Social Plugin