Na Said Mwishehe,Michuzi TV
Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Ndonga mkazi wa Majumbasita jijini Dar es Salaam amejikuta akipokea kipigo cha 'Paka mwizi' kutoka kwa wananchi wenye hasira kali baada ya kukwapua Biblia ya muumini wa dini ya Kikristo aliyekuwa akielekea Kanisani.
Tukio hilo limetokea leo Juni 7,2020, saa 12 asubuhi Njia Panda ya Segerea eneo la reli ambapo kijana huyo kabla ya kukwapua Biblia hiyo alitoa panga lake na kisha kumpiga na ubapa wa panga mgongoni muumini huyo aliyekuwa akielekea kwenye Ibada ya Jumapili.
Kwa mujibu wa mashuhuda wameiambia Michuzi Blog na Michuzi TV kuwa Ndonga alikuwa katika eneo hilo la relini akiendelea na mawindo na muda mfupi baadae alipita mtu kisha akamsalimia lakini inavyoonekana mtu huyo alishtuka hivyo akaamua kuongeza mwendo.
Hata hivyo, dakika chache baadae akapita muumini huyo mwanamke ambapo Ndonga alimuamkia yule muumini huku akimsogelea na kabla ya kukaa vizuri akashtukia akishambuliwa kwa kupigwa na ubapa wa panga.
Mmoja wa mashuhuda aliyekuwa eneo hilo la tukio amesema baada ya Ndonga kumpiga na ubapa wa panga muumini huyo alichukua Biblia ambayo ilikuwa ndani ya Pochi." Ujue kuna zile Biblia ambazo zinakuwa kama vile ziko kwenye pochi ambapo ukitaka kuifungua unafungua zipo na kisha yenyewe inakuwa ndani.Nadhani yule kibaka alijua muumini amebeba pochi tu."
Kwa mujibu wa mashuhuda baada ya kibaka huyo(Ndonga) kupora hiyo Biblia aliamua kuanza kuondoka kidogo kidogo kwa kufuata reli na wakati huo mwanamke aliyeporwa alibaki akipiga kelele za kuita "Mwizi ...mwizi... mwizi huyooo jamani".
Kelele hizo zikasababaisha baadhi ya vijana waliokuwa na bodaboda kumkimbiza ambapo walifanikiwa kumpata na kisha kumrudisha eneo la barabara ya kuingia mtaani.Hivyo wananchi wenye hasira kali walianza kumshambulia kwa mawe na magongo.
Kipigo kwa kibaka huyo kiliendelea kwani watu waliamua kujipigia tu hadi walipoona amepoteza fahamu kabisa na hajiwezi kwa lolote. Hata hivyo baadhi ya wananchi waliamua kuchukua majiwe makubwa na kumtwanga nayo usoni kiasi cha kuishiwa nguvu.Wapo wanaomini kibaka huyo amekufa ,hata hivyo ni Daktari pekee ndio mwenye uwezo wa kuthibitisha kifo.
Ingawa kwa wananchi wanaamini kibaka huyo ambaye alikuwa tishio kwa muda mrefu katika maeno ya Majumbasita, Kipawa,Karakata ,Sitakishari pamoja na eneo la Kuvuka reli atakuwa amekufa kutokana na kipigo alichokipata." Watu walikuwa na hasira naye sana huyu Ndonga.Amekuwa akipora watu kila siku na wengi wameachwa na majeraha mwilini kwasababu yake," amesema mmoja ya mashuhuda.
Kutokana na tukio hilo askari Polisi wa Kituo cha Stakishari walifika eneo la tukio na kisha kuuchukua mwili na kuondoka nao kwenye gari.Hata hivyo.mmoja wa askari alisikika akisema ndani ya wiki mmoja tayari ana kesi nane za watu waliokwenda kumtolea taarifa za kuporwa na kujeruhiwa na Ndonga.
Baadhi ya wananchi ambao wamezungumzia tukio hilo wamesema kwa sasa watakuwa na amani kwa kijana huyo alikuwa tishio na hawakuwa na furaha,hivyo sasa watapumzika ingawa Ndonga anao.mtandao mkubwa wa vijana wenzake ambao alikua akishirikiana nao kufanya matukio ya uhalifu.
Social Plugin