Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema uhuru wa Mahakama hauwezi kukamilika endapo watumishi wake hawatazingatia suala la uwajibikaji na Maadili mema.
Akifungua Mkutano wa Majaji wafawidhi na baadhi ya wajumbe wa kamati za Maadili kuhamasisha ufahamu wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama jijini Dodoma, Jaji Mkuu amesema uhuru wa Mahakama usioambatana na Uwajibikaji na Maadili ni uhuru ulio mashakani.
“Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ni mfano wa hatua madhubuti inayochukuliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kulinda uhuru wa Mahakama na wakati huo huo kuimarisha Uwajibikaji na Maadili” alisema Jaji Mkuu.
Kifungu cha 33(1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (Sheria Namba 4 ya mwaka 2011 kimeipa Tume ya Utumishi wa Mahakama uwezo wa kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwa Kamati zilioundwa chini ya Sheria hiyo ama zitakazoundwa na Tume.
Jaji Mkuu alisema Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama utaisaidia Tume hiyo kuzisimamia Kamati zilizokasimiwa mamlaka na pia utawezesha Kamati hizo kuwa na utaratibu unaofanana katika kufikia maamuzi.
Alizitaja Kamati zilizoundwa na Sheria Namba 4 ya mwaka 2011 kuwa ni Kamati ya Maadili ya Majaji (Judges’ Ethics Committee), Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama (Judicial Officers Ethics Committee), Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa na Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Wilaya.
Alisema Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya zimebeba dhana ya kutegemeana (inter-dependence) baina ya mihimili mitatu ya dola ili kuleta ufanisi katika shughuli za utoaji haki.
Aliongeza kuwa katika kutegemeana na kushirikiana, kila Mhimili unapaswa kufahamu Mamlaka na kazi za Mihimili mingine, kusaidiana, kulindana na kuteteana na Mihimili kutoingilia au kuvamia au kuchukua kazi au majukumu ya mihimili mingine.
Alisisitiza umuhimu wa Miongozo hiyo kusomwa na kueleweka ili iwasaidie Wahe. Majaji Wafawidhi, Mahakimu wote, watumishi wote wa Mahakama, Wenyeviti wa Kamati, na Wajumbe wa kamati za Maadili kutekeleza kwa vitendo dhana ya kutegemeana na kushirikiana.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Miongozo hii pia itaelimisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kufahamu majukumu ya Mahakama na kuhakikisha kuwa Kazi za Utoaji Haki haziingiliwi.
Aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapopokea malalamiko ya wananchi kuwaelimisha kuhusu mipaka ya mamlaka na kuwashauri utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Alisema Miongozo hii inaweka mizani kwa Jaji, Msajili au Hakimu anapotimiza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba, Sheria na misingi ya kiapo chake, asiingiliwe, asibezwe na asichukuliwe kuwa sio mzalendo hata pale uamuzi wake usipofurahisha. “Katika mizani, Jaji, Hakimu au Msajili hawako juu ya Sheria. Katiba na Sheria zimeweka utaratibu wa kupokea tuhuma dhidi ya viongozi hawa, kuzishughulikia, na hata kuwaondoa katika utumishi wa Mahakama.
Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Makama Kuu ya Tanzania kutoka kanda zote 16 nchini pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati za maadili walikutana kwa siku moja jijini Dodoma ili kujadili Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama.
Social Plugin